Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) ambalo ni msimamizi wa sekta ya Sanaa na burudani nchini linawakumbusha wamiliki na waendeshaji wa kumbi za burudani kufuata sheria, kanuni na taratibu walizopewa kwenye vibali vyao vya uendeshaji wa kumbi.
Wanaelekezwa kuhakikisha wanakuwa na vibali halali vya uendeshaji wa kumbi zao, kuzingatia muda wa utumizi wa kumbi, kuepuka kelele zinazosumbua kwenye maeneo maalum hasa makazi ya watu na kuhakikisha ulinzi na usalama wa maisha ya watu na mali zao.
Aidha, BASATA linawakumbusha wamiliki wote wa kumbi za sherehe na burudani kwamba ni marufuku kukusanya watoto katika kumbi zao kupitia kile kinachoitwa ‘Disko Toto’ katika msimu huu wa Sikukuu ya Christmas na Mwakampya ili kuepuka maafa yanayoweza kujitokeza.
Uzoefu unaonesha kwamba, nyakati za sikukuu kama hizi wamiliki wa kumbi wamekuwa wakijisahau na kuandaa madisko ya watoto hali mbayo imekuwa ikisababisha maafa ambayo yangeepukika kwa kufuata sheria, kanuni na taratibu.
Aidha, baadhi ya wamiliki na waendeshaji wa kumbi wamekuwa wakijisahau na kuendekeza faida pasi na kujali maelekezo ya vibali vyao wamekuwa wakijaza watu kupita viwango vya madaraja waliyopangiwa na BASATA.
BASATA kama mtoaji wa vibali vya kumbi za sherehe na burudani linasisistiza kwamba halitafumbia macho ukumbi wowote utakaokiuka maelekezo haya sambamba na kuruhusu maonesho machafu yenye kudhalilisha utu wa binadamu hasa yale yanayoonesha maungo ya ndani. Hatua kali na za kisheria zitachukuliwa kwa yeyote atakayekiuka maagizo haya.
BASATA linawatakia wasanii na wadau wote wa Sanaa Heli ya Christmas na Mwakampya
SANAA NI KAZI TUIKUZE, TUILINDE NA KUITHAMINI

Godfrey L. Mngereza
KATIBU MTENDAJI, BASATA

Post a Comment

Find Us On Facebook

TANGAZA NASI LEO