TASNIA ya Habari imepata pigo kubwa la kifo cha Mpigapicha mahiri, Mpoki Bukuku (44) aliyekufa leo asubuhi kutokana na majeraha ya kugongwa na gari eneo la Mwenge-ITV, Dar es Salaam jana.
Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya The Guardian Limited ambako Bukuku alikuwa akifanya kazi, Richard Mgamba alisema katika taarifa yake jana kuhusu kifo hicho kuwa, Bukuku alifariki katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.
Hata hivyo, taarifa za awali zilieleza kuwa Bukuku alifia katika Taasisi ya Mifupa Muhimbili (MOI) na Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano kwa Umma wa MOI, Almas Jumaa alithibitisha hayo kupitia taarifa mbalimbali za mitandao ya kijamii.
"Tumepoteza nguzo katika tasnia ya habari. Leo (jana) kama ilivyo kwa wengine wengi, nimepokea kwa mshtuko mkubwa na kutoamini, kuhusu kifo cha ghafla cha mmoja wa wapigapicha waandamizi wa The Guardian Limited, Mpoki Bukuku", alieleza Mgamba. Kwa mujibu wa Mgamba, Bukuku amefariki asubuhi.
Mgamba alisema katika familia yake, wamempoteza baba, mume na rafiki wa kweli, na kwa Kampuni ya The Guardian Limited, wamempoteza pia rafiki wa kweli na nguzo katika tasnia ya uandishi wa habari.
"Bukuku alikuwa ni mwanadamu tu kama ilivyo kwa yeyote kati yetu, lakini katika uandishi wa habari, alikuwa ni mtu aliyeipenda fani yake na hakuogopa kupambana alimradi apate habari nzuri. Ni kwa sababu hiyo ndiyo maana kuna wakati kiu yake ya kupata habari nzuri kuliko wengine wote ilimuweka matatani," alisema Mgamba.
Alisema Bukuku alikuwa na sifa zote za umahiri na utayari wa hali ya juu kupambana kupata habari picha iliyo bora na kwamba alikuwa shujaa na mwenye mapenzi na kazi yake hasa wakati akifuatilia habari kubwa kokote kule katika nchi hii.
"Bukuku amemaliza safari yake duniani, kimwili hayuko nasi lakini kiroho na kiweledi, mara zote atakuwa nasi daima. Sisi katika Kampuni ya The Guardian Limited tunaungana na familia, ndugu na marafiki katika kipindi hiki kigumu, kuombeleza msiba wa mtu ambaye tumekuwa tukifanya naye kazi kwa miaka mingi.
Kwa niaba ya wafanyakazi wote wa The Guardian Limited, kwa heshima kubwa natoa salamu zangu za rambirambi kwa mjane wa Bukuku, Lucy, watoto na wadau wote wa tasnia ya habari nchini, kwa kifo cha ghafla na cha kushtua cha mmoja wetu," alisema Mgamba.
Kwa upande wa Chama cha Wapigapicha za Habari Tanzania (PPAT) ambapo  Bukuku wakati wa uhai wake alikuwa ni mwanachama na mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya chama hicho, kimesema kimepokea kwa masikitiko makubwa kifo hicho cha ghafla cha Mpigapicha mwenzao.
Akizungumza na gazeti hili, Katibu Mkuu wa PPAT, Mroki Mroki, ambaye pia ni Mpigapicha Mwandamizi wa gazeti hili, alisema ni pigo kubwa kwa chama na wapigapicha wote wa habari nchini, kwani uzoefu wake katika kazi ulikuwa ukihitajika sana na wapigapicha chipukizi kujifunza.
“Licha ya kuwa alikuwa bado ni kijana lakini Bukuku alihitajika sana hivi sasa kutumia uzoefu wake katika kutoa elimu ya vitendo ya upigaji picha kwa vijana chipukizi wanaoibukia hivi sasa katika fani hiyo,” alisema Mroki.

Post a Comment

Find Us On Facebook

TANGAZA NASI LEO