Baadhi ya washiriki walikuwa wakijadili ripoti ya tathmini ya jinsi vyombo vya habari (televisheni, magazeti na redio) vilivyoripoti habari zao wakati wakitia nia na kugombea nafasi mbalimbali katika uchaguzi Mkuu wa 2015 na mjadala huo uliongozwa na  Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake (TAMWA).
Na fredy mgunda,iringa
MAKUNDI maalumu yanayohusisha vijana, walemavu na wanawake wa mjini Iringa walioingia katika mchakato wa Uchaguzi Mkuu wa 2015 wakitoa masikitiko yao ya namna vyombo vya habari vilivyowapa nafasi finyu katika mchakato huo.

Makundi hayo yalikuwa yakijadili ripoti ya tathmini ya jinsi vyombo vya habari (televisheni, magazeti na redio) vilivyoripoti habari zao wakati wakitia nia na kugombea nafasi mbalimbali katika uchaguzi huo iliyofanywa na Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake (TAMWA).

Dora Nziku anatoa malalamiko yake kwa kuvilaumu vyombo vya habari mkoani iringa kwa kutowapa nafasi wanawake,walemavu hata wale wasio na kipato kwa kuwa waandishi wengi walikuwa wanajali maslai kuliko ukubwa wa habari
“Naona kama wanawake tuliathiriwa zaidi katika mchakato huo kwani habari zetu hazikupata nafasi kama ilivyo kwa wagombea wengine hasa wanawake,” alisema Diwani wa Viti Maalumu Iringa Mjini, Dora Nziku (CCM).

Nziku alisema imekuwa ni jambo la kawaida kwa baadhi ya wanahabari kuomba hela kwa wagombea na viongozi wa kisiasa ili waweze kutoa habari zao.

“Pamoja na kuwapa hela wakati mwingine habari hizo hazitoki na mimi ni mmoja wa wahanga wa hilo, nimewahi kuita wanahabari, wakaniomba hela lakini hawakutoa habari zangu na nadhani hazikutoka kwasababu mimi ni mwanamke,” alisema diwani huyo bila kutaja wanahabari hao.

Naye Agusta Mtemi aliyekuwa mgombea udiwani viti maalumu mjini Iringa (CCM) alisema katika kinyang’anyiro hicho aliwashinda kwa kura 266 wagombea wenzake zaidi ya 10 lakini katika mazingira tata alionekana kama mshindi namba mbili na kukosa nafasi ya kuwawakilishi wanawake wenzake katika Baraza la Madiwani la Jimbo la Iringa Mjini.

Naye Imelta Mhanga kijana aliyegombea udiwani viti maalumu (CHADEMA) mjini Iringa alilaumu mchakato ndani ya chama akisema unawanyima uhuru wa kuongea na vyombo vya habari hasa wanapofanyiwa figisufigisu.

“Ndani ya taasisi kuna vitisho, kwamba shughuli za chama ni siri ya chama, hazitakiwi kutoka nje. Kwahiyo tunaogopa kukutana na wanahabari,” alisema huku akipinga kwamba wanahabari wanataka fedha mara zote ili kutoa habari zao.

Kwa upande wake, Selekti Sinyagwa ambaye ni mlemavu wa miguu aliyegombea udiwani viti maalumu ndani ya chama cha mapinduzi (CCM) alisema; “kwa kweli walemavu tunabaguliwa sana katika mchakato wa kupata viongozi, jambo hili linatufanya tujione kama ni jamii tofauti na jamii tunayoishi nayo.”

Afisa Miradi wa TAMWA, Reonida Kanyuma alisema taasisi hiyo iliangalia namna makundi hayo yalivyoripotiwa katika vyombo vya habari ili kwa kushirikiana na wadau waje na suluhisho litakaloondoa tofauti zilizopo.

“Tulifanya ufuatiliaji katika mchakato huo, na kuona jinsi wanawake, walemavu na vijana walivyoripotiwa katika vyombo hivyo vya habari ikilinganishwa na wagombea wanaume katika nafasi za udiwani, ubunge na urais waliopewa nafasi,” alisema.

Alisema kwa kuwa mwisho wa uchaguzi mmoja ni mwanzo wa uchaguzi mwingine, vyombo vya habari havipaswi kuwabagua wagombea kwa kuangalia udhaifu wao au mfumo dume na badala yake vitoe fursa sawa kwa kuzingatia uwezo na dhamira waliyonayo katika kuwatumikia watu wengine.


“Ni matarajio ya TAMWA na wadau wote wa maendeleo kwamba sekta ya habari itatenda haki kwa kutoa nafasi sawa kwa wagombea wote katika chaguzi zijazo,” alisema.

Post a Comment

Find Us On Facebook

TANGAZA NASI LEO