TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI *Ni kwa tuhuma za uzembe na upotevu korosho zaidi ya tani 2,000 * Wapelekwa Masasi chini ya ulinz...
TAARIFA
KWA VYOMBO VYA HABARI
*Ni kwa
tuhuma za uzembe na upotevu korosho zaidi ya tani 2,000
*
Wapelekwa Masasi chini ya ulinzi wakajibu tuhuma zinazowakabili
WAZIRI MKUU Kassim
Majaliwa amemwagiza Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Ruvuma, Kamishna Msaidizi wa
Polisi, Zuberi Mwombeji awakamate maafisa wanne na kuhakikisha wanapelekwa
Masasi chini ya ulinzi ili wajibu tuhuma za upotevu wa tani 2, 138 za korosho.
Maafisa hao ni Kaimu
Meneja Mkuu Chama Kikuu cha Ushirika cha Masasi (MAMCU), Bw. Kelvin Rajab na Meneja Tawi wa
MAMCU, Bw. Lawrence Njozi. Wengine ni wakurugenzi wa kampuni
ya YURAP ya Masasi inayohusika na uhifadhi wa mazao kwenye maghala, Bw. Yusuph
Namkukula na Bw. Ramadhani Namakweto.
Waziri Mkuu alifikia
uamuzi huo kwenye kikao alichokiitisha Songea mjini jana jioni (Jumamosi,
Januari 7, 2017) baina ya watendaji kutoka Bodi ya Korosho Tanzania, MAMCU,
wamiliki wa ghala la BUCO - Masasi na kikundi cha wakulima sita
waliowawakilisha wenzao kutoka vyama vya msingi (AMCOS) za wilaya za Mtwara na
Masasi.
Katika kikao hicho, Waziri
Mkuu alitaka apatiwe maelezo ya kina ni wapi zilipo hizo tani 2,138 za korosho
wakati taarifa waliyompatia viongozi hao jana inaonyesha kuwa waliuza korosho
zote na hakuna hata kilo moja ambayo haijanunuliwa katika mnada wa tano
uliofanyika Novemba 10, mwaka jana.
Kaimu Meneja Mkuu wa
MAMCU, Bw. Kelvin
Rajab alikiri mbele ya Waziri Mkuu kwamba korosho zote
ziliuzwa na zilishalipwa an wanunuzi wa mnda wa tano lakini akadai hakupewa taarifa
ya kukosekana kwa kiasi hicho cha korosho. Naye mmiliki wa ghala la BUCO, Bw. Ramadhan Namakweto alikiri kupokelewa kwa
korosho hizo ghalani kwake lakini akashindwa kutoa maelezo ni kwa nini
hazionekani zilipo.
“Tangu mnada wa tano,
mmekwishafanya minada mingine mitano hadi kufikia mnada wa 10. Kama kweli hizo
korosho zipo ghalani, ni kwa nini korosho za hawa wakulima hazijatolewa ghalani
na kuuzwa katika minada iliyofuata huku taarifa yenu ya fedha kuwa
mlishazipokea na kuziuza?” alihoji Waziri Mkuu bila kupata majibu ya kueleweka.
Tuhuma zinazowakabili
maafisa hao wanne ni kuwalipa kilo pungufu ya zile zilizowasilishwa ghalani,
wakulima wa korosho katika wilaya ya Masasi na kutowapa maelezo yoyote juu ya
upungufu huo. Mfano ni kufanya makato ya unyaufu kwa wakulima wa chama cha
msingi CHAMALI kinyume na maagizo ya Serikali.
Nyingine ni kutowalipa
fedha kwa wakati wakulima waliouza korosho kwenye mnada wa tano wa tarehe 10
Novemba 2016 na kutokutoa maelezo yoyote licha ya kuwa MAMCU ilishauza korosho
hizo kwenye minada iliyofuatia na kupokea malipo.
Nyingine ni kutopelekwa
mnadani kwa makusudi kwa tani 2,138 za korosho zilizokuwa katika maghala ya
Mtandi na BUCO tangu Novemba 11, mwka jana; kutokutolewa taarifa ya kuwepo
korosho hizo kwa mamlaka husika na kuwasababishia hasara wananchi.
Tuhuma nyingine ni
kushindwa kufuatilia malipo ya korosho ya tani 1,156,262 ambazo ziliuzwa kwenye
mnada wa 10 uliofanyika Desemba 21, 2016. Korosho hizo zilinunuliwa na Maviga
East Africa (tani 503,297); Machinga Transport (tani 104,200); Tastey (319,576)
na Saweya Impex (tani (229,189).
Kutokana na mapungufu hayo, Waziri Mkuu aliagiza
watu hao wapelekwe Masasi chini ya ulinzi ili uchunguzi ufanyike na pia amemuagiza
Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa
Hesabu za Serikali (CAG) afanye ukaguzi wa hesabu za MAMCU na
kujiridhisha kiasi cha korosho kilichonunuliwa; fedha zilizolipwa na kuingia
akaunti za MAMCU; kiasi cha fedha zilizolipwa kwa vyama vya msingi na wananchi
kwa ulinganifu na bei ya korosho kwa kila mnada husika.
Mapema, wakisoma risala yao kwa Waziri Mkuu, wakulima
hao walisema wana kero nyingi sana kama vile kutolipwa fedha zao kwa wakati;
kutoeleweka mahali zilipo korosho ambazo walishaziuza kwa MAMCU, kukatwa makato
ya unyaufu ambayo Serikali ilikwishapiga marufuku na kutosikilizwa malalamiko
yao na viongozi wa MAMCU pamoja na viongozi wa mkoa na wilaya.
“Makubaliano yalikuwa ni kwamba mkulima atapewa
fedha yake siku sita baada ya mnada kufanyika lakini hivi sasa baadhi yetu
tumeuza korosho tangu Oktoba, mwaka jana lakini hadi imefika Januari hii bado
hatujalipwa. Pia kuna makato yaliyoondolewa kwenye mfumo, kwa mfano unyaufu
lakini wao wameyaacha na unapoenda kuuza wanahesabu na kukukata kuwa utalipia
gharama za unyaufu,” alisema msoma risala Bw. Sylvester Mtimbe ambaye pia ni
mkulima kutoka AMCOS ya Chiungutwa.
Wakulima hao wa korosho kutoka Masasi mkoani
Mtwara walikutana Januari 3, 2017 katika kijiji cha Chiungutwa na kuazimia kuwa
wangeandamana hadi Dar es Salaam ili wawasilishe kilio chao kwa Waziri Mkuu au
kwa Mheshimiwa Rais Dk. John Magufuli.
Kwa kutambua umbali uliopo kutoka Masasi hadi Dar
es Salaam na kwamba yeye hakuwepo katika siku waliyopanga kwenda huko, Waziri
Mkuu aliamua kuwaita wakulima hao wamfuate Songea ambako alikuwa na ziara ya
kikazi ya siku nne.
(mwisho)
IMETOLEWA NA
OFISI YA WAZIRI MKUU
JUMAPILI, JANUARI 8, 2017.
COMMENTS