FILAMU iliyotengenezwa kwa kutumia simulizi la nyumbani na kufanyiwa foto katika maeneo ya uswahili hasa, yenye patashika la mapenzi iliyomhusisha Idris Sultani, Irene Paul, Ernest Napolean,Antu Mendoza na Akbar Thabeet inaingia rasmi sokoni kupitia majumba ya sinema Ijumaa wiki hii.

Filamu hiyo ambayo imepigwa maeneo ya Mburahati katika maeneo halisi ya watu wa hali ya chini ni simulizi la mapenzi lililojaa ubishi, misele na majanga kibao kabla ya wawili hawajapata nafasi ya kuoana.

Filamu hiyo ambayo ilioneshwa kwa waandishi wa habari leo kabla ya kuingia sokoni ni moja ya filamu kali iliyoandaliwa kwa namna ya kupandisha hadhi sinema za kitanzania.

Kutokana na uzuri na ubora wake katika skrini za  filamu, Kiumeni imepewa nafasi ya kutembea kwa wiki mbili katika jumba la sinema la Mlimani ikipata heshima yakuoneshwa kwa wandishi wahabari katika Holi namba moja.

Katika mchanganyiko wa waigizaji wapya yaani chipukizi na wakongwe akiwemo mzee muhogo mchungu ambaye alilazwa chini na mkewe kwa sababu za ugomvi za kifamilia, ilionesha umahiri mkubwa wa dairekta ambaye  alionesha close up zilizoenda shule na kuifanya filamu nzima kuwa na kiwango kingine kabisa.Ndani ya filamu Idris Sultan akicheza kama Gasper yeye ni Don ambaye anasambaza vitu vilivyokatazwa kwa watu (mihadarati) huku akiwa hana taabu na jeshi la Polisi, hali inaoyoonekana wakati akienda kutoa watu wake mahabusu wanakoshikiliwa.

Katika sinema hii Idriss amekuja kivingine kabisa, akionesha kazi ya matukio, akiwa hacheki lakini mwenye mamlaka ya mtu hatari, alikuwa ameuvaa uhalisia kikwelikweli. Huyu aliachwa na mpenzi wake wakati akitumbukia jela kutumikia kifungo baada ya kudakwa na mihadarati.

Aliporejea kimwana yuko Jijini tayari akiwa ameanzisha uhusiano na  Ernest Napoleon (Gue) mtoto wa tajiri ambaye dhiki kwao ni ulaji wa keki, si unajua simulizi lile la kama hawana mkate si wale keki  (ha ha ha).

Sinema inasemaje. Katika filamu hii unakutana na visa vya uswahilini. Lakini si kabla ya kuoneshwa adha ya kuwa na fedha na tabia ya kibri iliyooneshwa na Irene Paul ambaye alicheza kama Irene.

Ni simulizi lililojengwa katika mahusiano, simulizi ambalo mpaka mwisho unaweza kudhani kamba mambo yanaharibika lakini unakuja  kumalizia kwa furaha.

Baada ya kuonwa kwa simulizi hilo lenye aksheni waandishi wa habari walipata nafasi ya kuhoji washiriki ambao walionesha uhalisia wa ubebaji taswira kiasi cha kuonesha kwamba tupo karibu sana miaka mitano ijayo kuwa na tasnia nyingine.

Huhitaji kwenda shule kutambua kwamba muigizaji wa mara ya kwanza katika sinema Antu Mendoza akicheza kama Faith kwamba ni mdada wa kuja kumwangalia sana siku za usoni. Kama Lupita katika sinema yake ya  mwanzo, pasi shaka Antu amefanya vyema, sura matendo hayakuambatana na ugeni bali na wenyeji tosha katika tasnia.

Mchumba huyu wa Gue aliyefanikiwa kumtoa Gue kwao na kumpeleka uswahilini ambako kulizaa, visa vituko, masikhara, makavu, na kutukutanisha na  mchumba wake wa mwanzo (Gasper) aliyempeleka mbio Gue kwa lile penzi kunahitaji moyo mkubwa kuendelea kuishi kistaarabu.

Darekta  Nicholaus  (nick) Marwa anastahili sifa hasa katika sinematografa. Unaweza kusema kwamba  amekuwa na akili ya ziada katika sinema hii iliyotengenezwa kwa miezi mitatu na bajeti ya takribani  sh milioni 40 kwa mujibu wa projuza Napoleon ambaye pia amecheza nafasi ya Gue.

Amewapa nafasi kubwa waigizaji, nafasi ambayo pia unaiona katika skrini wakionesha sura zao na mambo yao wakizungumza nawe moja kwa moja, hii ndio sinema ambayo huwezi kuwa na shaka kwamba yoyote yule katika watu milioni 200 wanaojua kiswahili watakuwa na uhakika wa burudani.

Extras walitoka Mburahati ambako ilipigwa picha na Extras hawa ambao wote hawajui sinema walikuwa watu wazuri mno katika nafasi yao na hawakuonekana kubababaika.

Hii ndio unaiita sinema si ajabu imepewa wiki mbili katika jumba la sinema.

Sinema ya kwanza Napoleon ya Coming Bongo ilipewa siku moja lakini kutokana na mahitaji ilitembea wiki mbili na ndio maana projekti nyingine hii ya Kiumeni imepewa moja kwa moja siku nne , siku ya Primio ambayo ni kesho  sokoni kesho kutwa.


Post a Comment

Find Us On Facebook

TANGAZA NASI LEO