Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye amemshukuru Rais Dk Johna Magufuli kwa kipindi cha mwaka mmoja alichomuamini kutumikia wizara hiyo kama kijana.
Nape alisema hayo LEO jijini Dar es Salaam mbele ya Kanisa la Mtakatifu Peter ambako alikwenda kukutana na waandishi wa habari kwenye hoteli ya Protea hata hivyo mkutano huo kuzuiwa na jeshi la polisi hivyo kulazimika kuzungumza akiwa juu ya gari.
 “Lengo la kwangu la kuja hapa la kwanza ilikuwa ni kumpongeza Rais kwa uamuzi alioufanya na pia kumshukuru kwa kuniamini kwa mwaka mmoja, na wale mliotumwa sikilizeni mkawaambie,” alisema Nape.
Alisema anamshukuru Rais alimuamini kama kijana na kumpa heshima ya kuingia kwenye baraza la mawaziri na kwamba kama ambavyo Rais alimuamini atumikie kwenye nafasi hiyo lakini sasa ameona na amemuweka Aliyekuwa Waziri wa Katiba na Sheria Dk Harrison Mwakyembe.
Nape alisema anapongeza pia Dk Mwakyembe na pia anamuunga mkono  kwa uteuzi huo na kwamba kwasababu ni mwanahabari anaimani atasimamia vizuri tasnia hiyo.
Nape alisema hana kinyongo na Rais Magufuli katika uamuzi wake alioutangaza asubuhi jana wa kumteua Dk Mwakyembe kuwa Waziri wa wizara hiyo ambayo alikuwa akiiongoza yeye kushika nafasi yake.
“Kama ambavyo sikumshawishi Rais kunichagua ndivyo ambavyo sina say (kauli) na uamuzi aliofanya, lakini wakati anaunda baraza walikuwepo watu wengi sana, alipoamua kunichukua mimi kuna watu walikuwepo na walikubali, mimi leo nakatalia nini, sina sababu ya kukataa,” alisema Nape.
Baada ya Gari ya Nape kufika eneo la kanisa hilo wakati akishuka, alitokea mtu ambaye alianza kumsukuma Nape akimrudisha kwenye gari asishuke kwenda kuzungumza na waandishi wa habari ambao walikuwa wamejaa katika eneo hilo na baadaye kuja askari waliokuwa na sare.
Kitendo hicho cha Nape kusukumwa arudi kwenye gari na mtu yule aliyekuwa na nguo za kiraia ambaye Nape alisema hamfahamu na hajui ametumwa na nani Nape aliendelea kusisitiza kuwa hakuna haja ya kutumia nguvu na silaha akimtaka amuache aendelee kuzungumza na wanahabari.
Kutokutii huko kwa Nape kulimfanya mtu huyo ambaye alikuwa akimsukuma kulazimika kutoa silaha (bastola) akisisitiza Nape arudi kwenye gari.
Baada ya mvutano wa muda mrefu, Nape aliamua kusimama kwenye mlango wa gari na kuanza kuzungumza na wanahabari akiwa hapo na baadaye kuingia kwenye gari kufungua dirisha la juu ya gari akatoa kichwa na kuanza kuzungumza akiwa hapo huku wale watu waliokuwa wakimzuia wakiendelea kuwepo pale. 
Katika mazungumzo yake na wanahabari, Nape alisema amejitahidi kutimiza wajibu wake katika nafasi yake ya uwaziri.
“Jana wakati nilipoongea na vyombo vya habari wakati napokea ile ripoti, nilisema kuna gharama ya kulipa wakati wa kusimamia haki za watu na mimi niko tayari kulipa, sioni sababu kwanini vyombo vinapaniki,” alisema Nape na kuongeza kuwa  uzalendo wake kwa nchi hauwezi kutiliwa mashaka
“Nimekuwa mzalendo kwa nchi yangu, nimekuwa muungwana kwa nchi yangu na ninaapa kuendelea kuwa muungwana kwa nchi yangu hilo hakuna atakayelibadilisha,” alisema.
Alisema amekuwa pia mzalendo kwa CCM chama ambacho kiko kwenye shimo alisimama kukiinua uzalendo ambao haufai kutiliwa mashaka na kwamba alijifunza usemi wa ‘nitasema kweli daima fitina kwangu mwiko’ na alichokisimamia ni kusema kweli.
Alisema aliwataka watu hao waliokuwa wakimzuia pamoja na watu waliowatuma wasihangaike naye kwani ni mtu mdogo kuliko Tanzania badala yake wahangaike na mambo mengine yenye manufaa kwa nchi.
“Nimekuja hapa mtu anakuja na bastola ananiamrisha nirudi kwenye gari, nani amekupa mamlaka hayo, unalipwa kwa kodi ya kwetu, mnajua ni namna gani tumepambana kwaajili ya nchi hii, miezi 28 nalala porini angalieni mkono wangu huu,” alisema Nape.
Nape alisema hayo akionesha mkono ambao aliumia baada ya kupata ajali ya gari … ambapo alisema pia kuwa alipigana kuhakikisha Chama cha Mapinduzi (CCM) kinabaki madarakani.
Nape alisema vyombo vya ulinzi na usalama viangalie jambo hilo lililofanyika la kumzuia kushuka kwenye gari kwa kutumia nguvu na kummtolea bastola wakati hakuwa na nia mbaya.
“Nia yangu haikua mbaya kwa serikali yangu, nia yangu ilikuwa ni kuwaeleza watanzania kwamba maisha lazima yaendee, sasa wanapokuja watu wachache (wapuuzi) wanadhani wanaweza kukoroga hivi mambo,” alisema.
Alisema alipoteuliwa Rais John Magufuli hakumuuliza hivyo wakati anataka kumuweka mtu mwingine hana sababu ya kuulizwa na pia hana kinyongo na Rais.
“Sijasema chochote kwamba nina kinyongo na Rais wangu, kwani kuna watu wanataka wao ndio wawe waamuzi wa mawazo ya vijana wa nchi hii,” alisema Nape.
Aidha alisema kinachowakutanisha watu sio sare za CCM za rangi ya kijani bali imani ya kuwa wakweli kuachana na fitina.
Alisema uzalendo amefundishwa na baba yake marehemu Moses Nnauye ambaye alikuwa mwanasiasa mkongwe wa CCM kusema kweli na kusimamia anachokiamini na kama kitaleta matatizo hana shida kwani alishawahi kufukuzwa kwenye chama chake hicho.
Nape ambaye alishawahi kufukuzwa CCM alisema katika maisha ya siasa kupita kwenye migogoro ni jambo la kawaida kwani lazima mbegu ioze ndipo iote, “sasa mbegu niliyoipanda itaota, mbegu ya kusimamia haki hakika itaota.”
Aliwaasa vijana kusimamia ukweli, kutokuwa waoga na kusimamia kile wanachokiamini.
Nape alisema katika kipindi ambacho amekuwa katika wizara hiyo anaamini ametumia akili na uwezo wake wote kuwatumikia watu walioko chini na wizara hiyo na kwamba alipata ushirikiano wa kutosha.
“And I real love you people, napenda kufanya kazi na nyie na nimefurahi sana, sana kufanya kazi na nyie, na nina waombeni mumuunge mkono waziri mpya aliyepewadhamana na fanyeni nae kazi na pia endeleeni kumuunga mkono Rais Magufuli ndie rais tuliyepewa na Mungu na tuliyempigia debe watanzania,” alisema.
Aliwataka pia watanzania kuendelea kudumisha umoja na mshikamano wan chi na kwamba sio wakati wa kuvuruga nchi kwani kuna mambo mazuri mbele. lisema alipenda kuendelea kufanya kazi hiyo lakini wakati umefika amelazimika kuondoka
Nape alisema anarudi kufanya kazi katika jimbo lake kwa kuwatumikia katika yale waliyomtuma kama mbunge wao.Post a Comment

Find Us On Facebook

TANGAZA NASI LEO