Na abdul mtemvu

Ulimwengu wa siasa ulimalizika mwaka 2016 kwa kituko kikubwa cha aliekuwa rais wa Gambia, Yahya Jammeh, kwanza kukubali uchaguzi halali wa kidemokrasia kufanyika nchini kwake (hakulazimishwa na mtu yeyote).  Ukafanyika na akashindwa kihalali na, baadae mwenyewe,  kumpongeza aliemshinda (Adama Barrow), na dunia ikampongeza kwa kuwa muungwana wa kukubali matokeo. Dunia ilimpongeza kwa, pengine, kufikiria Afrika imejiingiza kwenye Ulimwengu wa demokrasia ya Kimagharibi. Kumbe sio! Yaliyotokea na kumkuta Yahya Jammeh ni historia, tofauti na heshima ambayo, pengine, angeipata kwa kukubali kwake kushindwa na kupata heshima iliyotukuka.
Mfano wake ni sawa na ule wa nchi ya Burkina Farso, ambayo iliinggia kwenye heka heka na misuko suko ya kijinga tu kwa Blaise Campaore kutaka kung’ang’ania madaraka! Sawa na yalioikumba Ivory Coast. Kisa, eti, ni wapambe  na ndugu hata marafiki walio karibu na kiongozi mhusika ambao hawako tayari kurudi kijiweni ilhali kuna lukuki ya wananchi wako kijiweni! Hawa ndio chimbuko la vurugu na machafuko yote! Wapambe nuksi. Nani asiejua Bagbo kaponzwa na nani? Alishindwa uchaguzi halali wa kidemokrasia nchini kwake na, baada ya kushindwa,  akashawishiwa na mkewe kuitumbikiza nchi yake kwenye machafuko makubwa ambayo hayana mithili. Leo, yuko wapi?  Hadithi kwa Afrika inaendelea na hakuna anaejifunza hadi kiyama kitukute.
Blaise Campaore (aliyempindua mwanamapinduzi wa mfano barani afrika na swahiba wake wa damu –Tomas Sankara),baada ya kunogewa na madaraka baada ya miaka takriban ishirini na saba madarakani  akakataa kuachia ngazi, huku akitaka kushawishi bunge kubadili katiba ili aendelee na uongozi wake usio na tija kwa nchi yake. Ya, Yahya  Jammeh ndio yalikuwa ya Blaise Campaore na ndio yaliyokuwa ya Bagbo! Hakuna aliejifunza kwa mwenzake?
Hawa ndio viongozi wetu wa bara letu ambao, kwa kiwango kikubwa, wengi wao wamechukua nafasi ile ile ya waliokuwa wakoloni wetu kupora rasilimali za nchi na, bila aibu, kuzipeleka  kule kule Ulaya! Neno demokrasia kwao ni msamiati tu usio maana wala tafsiri inayoeleweka. Demokrasia kwao ina tafsiri ya wao kuwepo madarakani, ama iwe kwa hila au ghilba. Alimradi na ikibidi wang’oke basi itakuwa ni kwa mbinde. Tena mbinde kweli kweli (wakati mwingine mpaka wazungu wawalazimishe). Kwao haijalishi madhara ama madhira gani wanasababisha kwa wananchi na nchi zao.
Aliekuwa rais wa awamu ya nne, Dk Jakaya Mrisho Kikwete, aliwashangaza mabalozi na wawakilishi wa Afrika, nchini China, wakati wa ziara yake nchini humo, alipozungumza kuhusu kuchoshwa na Urais na kutamani walau muda wake ungekuwa umeisha ili arudi nyumbani kuwa mtu wa kawaida! Rais Kikwete alizungumza hayo wakati hata muda wake wa mihula miwili ya miaka mitano mitano haijaisha rasmi. Wakati wa kuadhimisha miaka 53 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar, Tanzania na Dunia ilishuhudia viongozi wastaafu wa Tanzania (Mzee Mwiyi, Mkapa, Kikwete na Karume) wakiwepo kwenye membari wakicheka na kufurahi. Nchi gani Afrika ambayo  ina viongozi wastaafu wanaoweza kuwepo pamoja kwenye hafla ya kitaifa wakawa hawana bifu miongoni mwao? Wanacheka tu!
Blaise Campaore, kama mwenzake Yahya Jammeh,  alikaribia kumaliza miaka ishirini na saba ya utawala ambao wangalau ulikuwa na chembe chembe za kidemokrasia pamoja na kuwa alikuwa akiipinda pinda, baada ya awali kuingoza nchi yake kijeshi, lakini ni wazi kwa tamaa yake hiyo, miaka yote hiyo hayakumtosha. Angetaka, si angefanya katiba ya kuwa kiongozi wa maisha! Nani angeweza kumzuia, lakini hakuelewa. Hakuelewa kuwa katiba ndio imemponza. Katiba haichezewei chezewi kama kutafuna tambuu.
Hata hivyo, hii sio hoja ya msingi. Hoja ya msingi ni kwamba, kaifanyia nini nchi yake na watu wake miaka yote hiyo? Alimpindua Tomas Sankara (kama mwenzake Yahya Jammeh alivompindua kiongozi halali), lakini ilikuwa  yeye afanye nini? Ni wazi kuwa kilichompelekea kumpindua, na hatimae kumuua, rafiki yake na mwanamapinduzi mwenzake ni wivu na uchu wa madaraka. Hakusukumwa na mwamko kuwa mapinduzi yale, chini ya kapteni Sankara, yalikuwa yamekosa mwelekeo na kuwa Sankara alishapoteza dira na, kwa hali hiyo, akajiona yeye ndio alifaa kurekebisha mambo.
Hata pale alipomuua mwenzake dunia ilimsamehe. Viongozi wenzake wa Afrika (wakati ule hata Mwalimu Nyerere alimsamehe), waliangalia pembeni wakidhani, pengine, ni ajali ya kisiasa ambayo hutokea nyakati za vugu vugu za mapinduzi. Kumbe hakuwa na Uanamapinduzi wowote! Uchu na tamaa za madaraka ndizo zilizotawala udhalimu wake.
Ni kwa nini viongozi wetu (wa Afrika) hawaheshimu katiba? Ni kwa nini wanafikiri wananchi wao ni kundi sawa na la kondoo la kuburuzwa buruzwa tu, kundi la kudanganywa danganywa kila mara na wao ndio waamuzi wa mwisho wa mustakabali wa taifa na watu wao? Kama Blaise Campaore na  Yahya Jammeh  wameshindwa kuipa msukumo wa maendeleo nchi zao badala ya kujitajirisha wao, jamaa na familia zao tu, kwa miaka yote waliokaa madarakani, wangeweza kufanya nini kwenye miaka mingine wanayotaka kujiongezea - hata kama wangekaa daima madarakani.
Nchini Burkina Faso, na baadhi ya nchi zinazofanana nayo, wakati wa Campaore,  wananchi wa Ufaransa na wageni wengine waliishi maisha ya peponi kuliko hata Waburkinabe wenyewe ambao wengi wao wakilindwa na vikosi vya jeshi maalum la Ufaransa huku vijana (wasomi wa Kiburkinabe) wakiwa hawana matumaini yoyote ya hatma za maisha yao ya siku hadi siku. Maisha yasio matarajio ya ahueni kwa leo wala kesho! Huu na hii ndio dhana ya uhuru wa baadhi ya nchi zetu barani Afrika! Maisha na hali ambapo viongozi wamekua sawa na mwewe wanaovizia na kutafuna vifaranga vya kuku. Wanachuma utajiri unaoishia nchi za Ulaya. Kwao, wananchi wao ndio vifaranga na wao ndio mwewe!
Tony Blair, wakati akiwa madarakani, aliwahi kukaririwa akisema, kwamba: ‘Africa is not poor but is poorly governed’ dhana ambayo haina ubishi kwa kuwaangalia aina ya viongozi wengi barani kwetu. Kwa hakika, tumefika mahali, wazungu tunaowaenzi sana wamewafanya viongozi wetu wengi kuwa kama wanasesere wao! Nchi yoyote Afrika ambayo balozi wa Ulaya akiletwa na akikaa miaka miwili ndio anaishia kuwa mtaalam wa mambo ya Afrika nchini kwao.  Ni aibu! Bongo tuna watu wamekaa miaka hata ishirini vijijini wakiwa viongozi, lakini hatuna hata mtaalam mmoja ambae kaandika kitabu cha changamoto ya Wilaya ua Kijiji alichokiongoza! Mzungu anakuja nmiaka miwili tu, lakini mwaka mmoja tu anatoa darasa kwao! Anajiita mtaalam na hata kutufundisha sisi wenyewe wenye nchi yetu.
Hakika, tufike mahali viongozi wetu wabadilike. Kama mifumo ya kigeni imetushinda, basi, turudi ama tubuni mifumo itakayoendana na tamaduni na historia zetu. kwani kuna ulazima gani, mathalan, kuwa na vipindi vitano vitano vya mihula miwili vya Urais? Kwa nini tusifanye miaka kumi kumi ya vipindi viwili ili kiongozi atosheke ama hata kipindi cha muhula mmoja wa miaka kumi na ushee ya rais kutawala angalau atosheke yeye na wapambe wake? Mbona Papa, Kadinali au Mufti hawana muhula wa uongozi? Akitawazwa ni mpaka umauti umfike ndio aje mwingine.
Ili balaa la viongozi wetu kutaka katiba iseme mihula ya utawala katuletea nani wakati hatuiheshimu? Iweje, viongozi wetu wanaoridhia balaa hili la kutaka mihula ndio hao hao wawe chanzo cha machafuzi ya nchi zetu? hakika, ipo haja ya kutafakari ili.
Wasalaam.


Post a Comment

Find Us On Facebook

TANGAZA NASI LEO