RAIS Dk. John Pombe Magufuli anatarajiwa kuwa, mgeni rasmi katika maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari duniani (WPFD).
Maadhimisho hayo yatahudhuriwa na watu wapatao 250 kutoka ndani na nje ya nchi yatafanyika katika hoteli ya Malaika, mkoani Mwanza Mei 2 na 3, mwaka huu.
Hii itakuwa ni mara ya kwanza kwa Rais Magufuli kushiriki katika hafla ya wana habari tangu ameingia madarakani mwishoni mwa mwaka 2015.
Akizungumzia kuhusu maadhimisho hayo kwenye mkutano na waandishi wa habari Jijini Dar es Salaam, Kaimu Mwenyekiti wa Taasisi ya Vyombo vya Habari Kusini mwa Afrika, tawi la Tanzania (MISA TAN), Kaimu Mwenyekiti wa taasisi hiyo Salome Kitomari alisema ni jukwaa linalotumiwa na wadau wa vyombo vya habari kuweka msukumo kwa mataifa kutunga sheria rafiki za vyombo vya habari zinazohakikisha uhuru wa habari katika nchi husika.
Ameeleza kuwa, suala hilo litafanywa kwa kujadili lengo likiwa kufikia makubaliano ya kitaifa kuhusu kuanzisha utaratibu wa ulinzi na usalama wa wanahabari na wafanyakazi wa vyombo vya habari kwenye mtandao nan je ya mtandao kutetea sera na mfumo wa mgeuzi kwa ajili ya vyombo vya habari na maendeleo endelevu.
Kwa mujibu wa Kitomari ushirikiano wa pamoja kwa ajili ya maadhimisho ya kitaifa ya siku ya uhuru wa habari duniani una lengo la kuimarisha utekelezaji wa pamoja wa mfumo wa kisheria na udhibiti unaofaa, mahusiano katika utekelezaji ili kuongeza upatikanaji wa habari na uhuru wa kujieleza.
Maadhimisho ya WPFD mwaka huu yanafanyika huku vyombo vya habari na wanahabari nchini vikibiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo baadhi ya vyombo kupunguza wafanyakazi kutokana na kushuka kwa biashara, uvamizi wa ofisi za vyombo vya habari na kupigwa kwa wanahabari wakiwa wanatekeleza majukumu yao.
Mwenyekiti wa MISA TAN ameeleza kuwa, katika maadhimisho yatakayofanyika mwaka huu wahanga wa ukiukwaji wa uhuru wa habari watatoa ushuhuda kuhusu changamoto walizokutana nazo.
Akizungumza katika mkutano huo Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri (TEF) Theophil Makunga alisema umefika wakati kwa waandishi wa habari kuyapa kipaumbele mambo yanayowagusu badala ya kuona kwamba hayawahusu.
Naye Raziah Mwawanga kutoka Tanzania Media Foundation alieleza kuwa, uhuru wa vyombo vya habari ni jambo muhimu hasa kutokana na mwenendo ulioanza kutojitokeza hapa nchini na kwamba ili mwandishi afanye kazi yake anahitaji uhuru.
Source: Said Mmanga

Post a Comment

Find Us On Facebook

TANGAZA NASI LEO