Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) Dkt. Albina Chuwa akimuhoji mmoja wa wakazi wa kijiji cha Chonyonyo wilaya ya Karagwe mkoani Kagera kuhusu jinsi zoezi la Utafiti wa Viashiria na Matokeo ya UKIMWI  lilivyofanyika katika kaya yake. Mahojiano hayo yamefanyika  wakati  Mkurugenzi Mkuu huyo wa NBS alipofanya ziara mkoani humo hivi karibuni kuangalia jinsi zoezi la utafiti huo linavyoendelea

Imeelezwa kuwa asilimia 97 ya watanzania wanaoishi katika kaya zilizochaguliwa kwa ajili ya Utafiti wa Viashiria na Matokeo ya UKIMWI katika mikoa 11 ambayo imeshafikiwa hadi sasa,  wameshiriki kikamilifu katika utafiti huo unaoendelea kufanyika nchini.
Hayo yamesemwa hivi karibuni na Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) Dkt. Albina Chuwa wakati akitoa taarifa ya utekelezaji wa utafiti huo kwa Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Kagera Wambura Sabora alipofanya ziara mkoani humo kuangalia jinsi zoezi la utafiti huo linavyoendelea.
"Ninayo furaha kukutaarifu kwamba,  mpaka sasa utafiti huu umeshafanyika katika mikoa 11 ya Tanzania Bara pamoja  na visiwa vyote vya Zanzibar yaani Pemba na Unguja.  Jambo la kufurahisha zaidi ni mwitikio wa wananchi ambao ni asilimia 97 ya wanaoishi katika kaya zilizochaguliwa kwa ajili ya utafiti kukubali kushiriki," amesema Dkt. Chuwa.
Mikoa ambayo imekamilisha utafiti huu wa Viashiria na Matokeo ya UKIMWI ni pamoja na Singida, Dodoma, Manyara, Iringa, Njombe na Ruvuma. Mikoa mingine ni Mbeya, Songwe, Katavi, Tabora na Kigoma.
Nae Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Kagera Wambura Sabora amemwambia Mkurugenzi Mkuu wa NBS kwamba, zoezi la utafiti huo mkoani humo linaendelea vizuri na mpaka sasa hakuna tatizo lolote  lililoripotiwa ofisisini kwake.
"Nami nichukue fursa hii kukueleza kwamba zoezi hili linaendelea vizuri hapa mkoani Kagera na mpaka sasa hakuna shida yoyote iliyojitokeza. Aidha, maeneo ya Kerwa, Missenyi na Wilaya ya Bukoba tayari yamekamilisha utafiti huu", amesema Sabora.
Kwa upande wake  mmoja wa wakazi wa kijiji cha Chonyonyo wilaya ya Karagwe mkoani Kagera aliyehojiwa na Mkurugenzi Mkuu wa NBS Dkt. Albina Chuwa kuhusu jinsi alivyoshiriki kwenye utafiti huo, alisema amefurahishwa na utafiti huo kwa kuwa amepata fursa ya kupima vipimo mbalimbali ambavyo hakutarajia kuvipata vyote kwa wakati mmoja.
"Kwakweli nimefurahishwa na utafiti huu kwakuwa sikutarajia kupima vipimo vya magonjwa ya Homa ya Ini, Kaswende pamoja na UKIMWI kwa wakati mmoja nikiwa nyumbani kwangu," ameeleza Mkazi huyo wa kijiji cha Chonyonyo.
Utafiti huu wa Viashiria na Matokeo ya UKIMWI Tanzania unaendeshwa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) kwa kushirikiana na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Tanzania Bara, Wizara ya Afya kwa Tanzania Zanzibar, Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali, Zanzibar (OCGS), Tume ya Taifa ya Kudhibiti UKIMWI (TACAIDS) na Tume ya UKIMWI Zanzibar (ZAC).
source Veronica Kazimoto
Bukoba
10 Aprili, 2017.Post a Comment

Find Us On Facebook

TANGAZA NASI LEO