Katika kuendeleza falsafa ya kupinga rushwa na matumizi mabovu ya fedha za umma kiongozi wa mbio za mwenge wa uhuru kitaifa mwaka huu Amour Hamad Amour amegoma kuzindua mradi wa maji wa Mkako uliopo wilaya ya Mbinga mkoa wa Ruvuma
Aliwaeleza wananchi waliokusanyika katika eneo la mradi kuwa  malengo ya mwenge wa uhuru ni kusaidia jitihada za serikali ya awamu ya tano kuwaondolea umasikini na ugumu wa maisha watu wake
Mradi wa maji wa kijiji cha Mkako ulianza kutekelezwa mwaka wa fedha 2014/2015 ambapo mkataba ulipaswa kukamilika ndani ya miezi sita kwa gharama ya shilingi milioni mia saba kumi na nane
Kiongozi wa mbio za mwenge wa uhuru kitaifa alieleza kusikitishwa na mradi wa maji wa Mkako kuwa umechafua taswira nzuri ya wilaya ya Mbinga ambayo awali aliisifia kwa kupiga hatua kubwa ya maendeleo
Amour alisema mradi umekaa muda mrefu mno  tangu uanze mwaka 2014 kwani ulipaswa kuwa umekamilika  baada ya  miezi sita na cha ajabu “fedha zimeliwa na  watu wapo ofisini hadi leo”.
Akitoa taarifa ya mradi huo kwa kiongozi wa mbio za mwenge kitaifa  mhandisi wa Halmashauri ya wilaya ya Mbinga Vivian Mndolwa alieleza kuwa tayari mradi huo umetumia shilingi milioni mia sita thelasini na nne  na kwamba umekamilika April mwaka huu
Aliongeza kusema mradi huu umekuwa na changamoto kubwa za uharibifu wa vyanzo vya maji baada ya usanifu hali inayopelekea maji kupungua na kutoka machache
Mhandisi Mndolwa aliongeza kusema  sababu nyingine iliyopelekea mradi kuchelewa kukamilika  ni kupasuka kwa mabomba kutokana na maji kuwa na nguvu kubwa ya msukumo hali iliyolazimu mkandarasi atumie teknolojia mbadala ya kuunga mabomba  kwa umeme
Pamoja na sababu alizotoa mhandisi  Mndolwa , kiongozi wa mbio za Mwenge kitaifa Amour Hamad Amour alihoji  kutochukuliwa hatua kuwasaidia wananchi kupata maji mapema
Amour alisema wao kama wakimbiza mwenge wa Uhuru Kitaifa wanazo taarifa kuwa mradi huu umetekelezwa chini ya kiwango hali inayowasababishia wananchi kukosa maji licha ya serikali kutoa fedha nyingi
“Hatuwezi kumwakilisha Rais kwenye mradi ambao haijakidhi viwango na kukosa tija iliyotarajiwa na watu kwani tatizo la maji ni kubwa katika kijiji cha Mkako” alisema Amour
Alisema Rais hawezi kufungua mradi usio na viwango kwani mwenge  wa Uhuru upo kwa niaba ya Rais
Kiongozi  huyo wa mwenge wa Uhuru kitaifa aliongeza kusema kuwa wamepata taarifa kuwa kabla ya kufika kwenye mradi wa Mkako kuwa wahusika walibeba maji kwenye magari na kuyaweka ndani ya tenki kubwa ili ionekane wananchi wanapata maji
Kufuatia udanganyifu aliojionea kwenye mradi huu Amour alimwagiza mkuu wa wilaya ya Mbinga Cosmas  Nshenye kuunda kamati ya uchunguzi mapema iwezekanavyo ili kupata ukweli wa tatizo la mradi huu kutokamilka kama makataba ulivyowekwa.
“Taarifa ya uchunguzi wa mradi huu itakapokamilika tunataka iwasilishwe kwenye ngazi zote za mamlaka husika ili watumishi na mkandarasi aliyehusika sheria ichukue mkondo wake” alisema Amour
Amour alionya dhidi wa watendaji na viongozi wanaoendelea kujihusisha na vitendo vya ufisadi na rushwa kuwa serikali ya awamu ya tano chini ya Rais John Pombe Magufuli imejipanga kuwafichua na kuachukulia hatua kali za kisheria
Kwa upande wake Mkuu wa wilaya ya Mbinga Cosmas Nshenye amekiri kuwepo kwa udhaifu kwenye mradi wa maji Mkako na kuahidi kuwa atachukua hatua za kuunda timu ya uchunguzi haraka kama alivyoelekeza kiongozi wa mbio za mwenge wa uhuru mwaka huu.
“Hili suala nitalisimamia kwa kuhakikisha huyu mkandarasi tuliyempa kazi  na kushindwa anachunguzwa na hatimaye hatua za kisheria zitachukuliwa.Tutaleta taarifa za utekelezaji wa agizo hili” alisema mkuu wa wilaya ya Mbinga.
Mwenge wa uhuru ukiwa Halmashauri ya wilaya ya Mbinga umeweza kutembelea,kukagua na kufungua jumla ya miradi tisa ya maendeleo pamoja na kuelimisha wananchi kwenye mikutano  juu ya kauli mbiu ya mwaka huu isemayo “Shiriki kukuza uchumi wa viwanda kwa maendeleo ya Taifa”


Post a Comment

Find Us On Facebook

TANGAZA NASI LEO