KAMISHINA  wa Bima nchini, Dk Baghayo Saqware  amesema kukosekana kwa sera ya taifa ya Bima nchini ni moja ya sababu kubwa ya kuendelea kudorora kwa sekta hiyo kwa upande wa afya.
Dk Saqware alisema hayo katika kongamano la kwanza la Afya bora kwa wote lililofanyika Jijini Dar es salaam jana.
Alisema kuwepo kwa sera ya bima kutatoa mwelekeo wa pamoja kwa masuala mengi yakiwemo matumizi ya tehama katika madai na malipo na pia ulinzi kwa wapewa huduma hali ambayo inachochea huduma bora kila mahali na hivyo wananchi kuona umuhimu wa kuwa katika mfumo wa bima.
Katika kongamano hilo lililoshirikisha watumishi wa sekta ya afya, watafiti, wanazuoni na wataalamu wa masuala ya bima,lilijadili mada zaidi ya 15 na lilifanyika chini ya mwavuli wa ushirikiano kati ya sekta ya umma na sekta binafsi (Public Private Partnership).
Dk Saqware alisema ukosefu wa sera ni sehemu ya matatizo makubwa ambayo yanayosababisha kutotanuka kwa sekta ya afya kupitia bima.Aliyataja matatizo mangine kuwa watoa huduma kutumia vibaya raslimali za bima kwa namna ambayo inaonekana kama kuwakomoa wateja.Aidha huduma ya bima imekuwa haiaminiki pamoja na kuwepo kwa sheria ya kuwezesha kuwapo kwa bima ya afya.
Alisema ili kufanikisha utoaji wa huduma kwa haki, kati ya sekta binafsi na ya umma kuwapo kwa sera kutasaidia kuwapo kwa mwongozo wa namna ya kutoa huduma na kulinda watumiaji wake.
Aidha sera hiyo ndiyo itakayoshughulikia pia wale ambao wanaotoa huduma kwa kukomoa na kusababisha bima kuonekana ya hovyo na isiyoaminika.
Alisema sera pia ingeliweza kusaidia  kurejesha thamani ya bima miongoni mwa wananchi walikokata tamaa na hivyo kuanzisha mikakati ya watu kutambua na kuithamini bima katika sekta ya afya.
Kongamano hilo ambalo limefanyika katika kipindi ambacho taifa linajiandaa kuhakikisha kila mtanzania anakuwa na uhakika wa kupata huduma za matibabu kupitia bima ya afya lilikuwa na washiriki zaidi ya 250 wakitoka Uholanzi,Kenya, Afrika Kusini,Ghana na Tanzania.
Mmoja wa waandaji wa kongamano hilo Dk Heri Marwa kutoka Shirika la PharmAcess alisema washiriki hao ni kutoka makundi mbalimbali ya kijamii, utendaji na usimamizi na wawakilishi kutoka Serikalini.
Kongamano hilo ambalo limeandaliwa kwa pamoja kati ya Mamlaka ya Usimamizi wa Bima nchini (TIRA) na Shirika la PharmAccess linalosimamia huduma ya Mfuko wa Afya ya Jamii ulioboreshwa katika mikoa ya Kilimanjaro na Manyara kazi ambayo PharmAcess wanafanya kwa kushirikiana na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) lilifunguliwa na Mwenyekiti wa Bodi ya wakurugenzi ya Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya, Anne Makinda.
Mada zaidi ya 15 zilizotolewa zililenga kujenga uelewa wa pamoja kuhusu hatua iliyofikiwa na Serikali kuelekea afya bora kwa wote na umuhimu wa wadau mbalimbali kuunga mkono jitihada hizo. Washiriki katika mazungungumzo ni pamoja na  Dk Anna Nswilla kutoka Tamisemi, Nina Siegert kutoka Uholanzi, O’Dougherty kutoka USAID na Profesa Angwalla Kiwara.
Washiriki walipata fursa kubadilisha uzoefu katika maeneo muhimu ambayo ndio dira kuu ya kuelekea afya bora kwa wote yanayohusu; kuongeza uwigo kwa makundi mbalimbali hasa sekta isiyo rasmi, umuhimu wa huduma bora na masuala ya TEHAMA pamoja na umuhimu wa utafiti katika kufanikisha huduma bora.
Mwisho. 

Post a Comment

Find Us On Facebook

TANGAZA NASI LEO