>>>Katavi wachimbaji, walinzi wapambana

JESHI la Polisi mkoani Shinyanga limelazimika kupiga mabomu ya machozi na maji ya kuwasha kwa kundi la waendesha bodaboda zaidi ya 80.
Watu hao walikuwa wakiandamana katika eneo la Ibinzamata baada ya mwenzao, Joel Mamla (26) kupoteza maisha juzi wakati alipokuwa anapelekwa  Kituo cha Polisi mjini Shinyanga baada ya kuvunja sheria za barabarani.
Jeshi hilo lililazimika kutumia kikosi cha Askari wa Kutuliza Ghasia (FFU) kutuliza vurugu hizo, ambapo walitumia ‘section’ tano za askari, ambapo kila ‘section’ yenye askari tisa ilitumika kuwatuliza waendesha bodaboda hao baada ya kuwataka watawanyike kwa amani.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, Jumanne Murilo, alithibitisha kutokea kwa vurugu. Alisema waliamua kuzuia maandamano hayo kwa kutumia mabomu kwa sababu urushaji wa mawe uliokuwa ukifanywa, ulionekana kuhatarisha hali ya usalama.
Alisisitiza kuwa maandamano hayo siyo si halali, na bodaboda hawakupaswa kufanya hivyo, bali walitakiwa kutii sheria bila shuruti, na kufuata taratibu za kudai kuonewa, na siyo kutishia kuharibu amani.
“Tulishaacha ule ukamataji wa bodaboda kwa kuwakimbiza, kwa sasa anapovunja sheria tunamfuatilia taratibu na kumkamata kwenye mazingira ambayo hayawezi kuhatarisha maisha yake,” alisema.
“Aliyefariki alifanya makosa na askari wetu wa usalama barabarani Koplo Lwehendela alimfuatilia mpaka akamkamata na alikubali makosa na kukubali kwenda kituo cha polisi. Baada ya kukubali, Lwehendela alimuelekeza Konstebo Edmond ambaye ni askari wanaovaa kiraia afuatane naye hadi kituoni.
“Lakini alitumia ujanja na kumweleza askari kuwa pikipiki ina matatizo hivyo askari apande ili waweze kuelekea kituoni, walipokuwa njiani ndipo dereva huyo alipokuwa kwenye barabara inayoelekea Tabora- Tinde, ndipo dereva huyo alipoongeza kasi ya pikipiki huku akiiyumbisha barabarani na alikuwa akimwambia askari wetu kuwa lazima wafe wote.
“Aliendelea kwenda kwa kasi huku wananchi wakiwa wanashangaa nini kilichotokea, ghafla waligonga nguzo pembeni ya barabara maeneo ya Huangija na kuanguka kwenye shimo, ndipo alipofariki dereva na askari wetu kujeruhiwa vibaya”, alisema.
Kamanda huyo alisema baada ya ajali hiyo juzi, jana walipata taarifa kuwa kuna mwanasiasa (jina wamelihifadhi) ambaye anadaiwa kuwahamasisha waendesha bodaboda takribani 1,000 kuandamana wakidai kuuawa. “Kuna mtu alikuwa anashinikiza madereva wafanye maandamano, lakini wengi wa madereva hao walionekana kutokubali na badala yake takribani 80 walifanya alivyokuwa amewaambia.”
“Tulipambana nao na tuliweza kurudisha amani. Na kwenye mchakato huo walipasua kioo cha mbele cha gari letu lenye namba PT 3705 kwa mawe waliyokuwa wakirusha. Lakini jeshi letu liliweza kuwakamata 28 na pia walikamata pikipiki 86 baada ya waandamanaji kukimbia na kuziacha,” alisema Murilo.
Taarifa za awali za tukio hilo, zinaeleza kuwa jeshi hilo lilitumia takribani saa sita ili kuwatawanya waendesha bodaboda hao, waliokuwa wakiandamana huku wakirusha mawe, kupinga kitendo cha mwenzao kufa wakidai kifo hicho kimesababishwa na askari polisi.

Hata hivyo, mshangao uliibuka kwa wananchi wa manispaa ya Shinyanga baada ya baadhi ya askari wa kikosi cha kutuliza ghasia, kuwatawanya waombolezaji waliokuwa katika msiba wa Mamla, kwenye nyumba aliyokuwa akiishi dereva huyo jana na kuzua taharuki zaidi.
Baadhi ya waendesha bodaboda, Simoni Bundala na Ramadhani Faraji walisema wameamua kuandama kwa madai ya kutaka kufikisha ujumbe ili serikali ione Polisi mkoani Shinyanga  isivyotenda haki, bali linawaonea.

Faraji alisema haiwezekani askari aliyevaa kiraia akamate pikipiki yenye makosa bila hata ya kuonesha kitambulisho, jambo ambalo ni hatari kwa kuhofia unyang'anyi wa pikipiki.

“Tukio la juzi bodaboda mwenzetu Joel (Mamla) mkazi wa mjini humo alikufa katika ajali iliyosababishwa na askari aliyemkamata kumkaba shingo hadi kusab
abisha ajali wakati akimlazimisha kwenda kituo cha polisi," alisema Bundala. 

Huko Mpanda, vurugu zimeibuka katika machimbo ya madini ya dhahabu  ya Isumamilo wilayani Mpanda katika mkoa wa Katavi  baina ya wachimbaji wadogo wapatao 6,000 na walinzi wa machimbo na kusababisha kibanda cha kupimia madini hayo  na ofisi kuchomwa na kuteketea kwa moto.
Kufuatia  vurugu hizo, walinzi wa machimbo hayo walilazimika kufyatua risasi za moto hewani  ili kuwatawanya wachimbaji hao wadogo.
Kaimu Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Katavi, Benedict Mapujila amethibitika kutokea kwa tafrani hiyo na alisema vurugu hizo zilidumu zaidi ya saa moja zilitokea  jana  saa 2:30 asubuhi.
Alisema kuwa hadi sasa hakuna  mtuhumiwa yeyote  aliyekamatwa  wala hakuna  mtu yeyote aliyepoteza maisha na Polisi inaendelea na uchunguzi wa tukio hilo.
Mapujila alisema vurugu hizo zilisababishwa  na walinzi wa machimbo hayo, kumkamata mchimbaji mdogo wa madini ya dhahabu akiwa na madini hayo akitaka kutoroka.
“Baada ya mchimbaji huyo mdogo wa madiniya dhahabu  kukamatwa na walinzi hao kumshambulia kwa kumpiga  mateke na marungu kitendo ambacho kiliwakasilisha  wachimbaji wenzake wakilalamika kuwa imekuwa ni tabia  ya walinzi wa machimbo hayo kuwapiga wachimbaji," alieleza Mapujila.
Akisimulia mkasa huo, alisema kuwa kundi kubwa la wachimbaji hao wadogo wakiwa na hasira, walijikusanya na kuanza kuvamia kibanda cha walinzi na ofisi ya kupimia madini hayo na kuteketeza kwa moto.
“Wakati wachimbaji hao  wakiteketeza kibanda hicho  kwa  moto walinzi wa machimbo hayo walilazimika kufyatua risasi za moto  hewani lakini  wachimbaji hao  hawakujali   waliendelea   bila   kujali risasi,” alieleza Kaimu Kamanda huyo.
Mkuu  wa   Mkoa  wa   Katavi, Raphael Muhuga   alifika  kwenye   eneo  hilo na kusikiliza kero  mbalimbali zilizotolewa na wachimbaji hao wadogo na aliwataka wafuate  taratibu  zilizowekwa na Serikali kulalamika.
“Kiitendo cha  wachimbaji kutorosha   dhahabu   bila  kupima kunasababisha  Serikali kukosa  mapato  yatokanayo na madini hayo," aliwaeleza.
Machimbo ya  Isumamilo  yamekuwa  maarufu kwa kipindi cha  miezi minne  sasa kutokana na kugundulika kwa dhahabu nyingi. Wachimbaji  wadogo  6,000  kutoka mikoa mbalimbali nchini hususani ya Kanda ya Ziwa, huchimba madini hapo.
Source:HabariLeo

Post a Comment

Find Us On Facebook

TANGAZA NASI LEO