HOTUBA YA MHESHIMIWA KASSIM M. MAJALIWA (MB), WAZIRI MKUU WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, WAKATI WA KUAHIRISHA MKUTANO WA SABA WA B...
HOTUBA YA MHESHIMIWA KASSIM M.
MAJALIWA (MB), WAZIRI MKUU WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, WAKATI WA
KUAHIRISHA MKUTANO WA SABA WA BUNGE LA KUMI NA MOJA LA JAMHURI YA MUUNGANO WA
TANZANIA TAREHE 05 JULAI, 2017
UTANGULIZI:
1.
Mheshimiwa
Spika, leo tumefika mwisho wa
Mkutano wa Saba wa Bunge la 11 ulioanza Jumanne ya tarehe 4 Aprili, 2017.
Tunayo kila sababu ya kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutuwezesha kuifikia siku hii, tena baada ya kuwa
tumetimiza wajibu wetu wa Kikatiba kikamilifu na kwa umahiri mkubwa. Huu
ulikuwa ni Mkutano muhimu sana kwa nchi yetu kutokana na jukumu kubwa la
kujadili na kupitisha bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 ulioanza
tangu tarehe 1 Julai, 2017. Bajeti hii ambayo ni nzuri na ya kihistoria ni ya
pili tu kati ya takribani Bajeti tano za Serikali ya Awamu ya Tano
zitakazoandaliwa hadi kifikia Mwaka wa Fedha 2020/2021.
2.
Mheshimiwa
Spika, wakati Bunge lako likiendelea, tarehe 13
Aprili, 2017 tulipokea kwa mshtuko na masikitiko makubwa taarifa za vifo vya
askari polisi wetu 8 waliopoteza maisha wakiwa wanalitumikia Taifa kwa kuuawa
na kundi la wahalifu katika eneo la Jaribu Mpakani, Wilayani Kibiti mkoani
Pwani. Askari hao waliopoteza maisha ni Inspekta Msaidizi Peter Kiguu, Koplo
Francis, PC Haruna, PC Jackson, PC Zakaria, PC Siwale, PC Maswi na PC Ayoub. Pia,
hivi karibuni mwezi Juni, 2017 Askari wetu wawili wa Kikosi cha Usalama
Barabarani walivamiwa na kupigwa risasi na majambazi katika Kijiji cha Bungu
“B” kilichopo Wilayani Kibiti. Aidha, wananchi wetu wengi wamepoteza maisha
kutokana na uhalifu unaofanywa na majambazi waliopo katika maeneo ya Kibiti,
Rufiji na Mkuranga.
3.
Mheshimiwa Spika, natumia fursa hii kulaani
kitendo hicho cha kihalifu, na kutoa pole kwa Inspekta Jenerali wa Polisi kwa
kuondokewa na vijana hao shupavu. Aidha, natoa pole kwa familia za wafiwa wote
kwa kuondokewa na wapendwa wao. Mauaji ya Wananchi wetu na askari wetu
hayakubaliki na wala hayavumiliki, kwani Askari ndio walinzi wetu sisi pamoja
na mali zetu. Aidha, tishio kwa walinzi wa amani na wananchi wetu ni tishio
kwetu sote, hivyo, Serikali itahakikisha waliohusika na mauaji hayo wanakamatwa
na kuchukuliwa hatua stahiki. Wanaweza
kukimbia, lakini hawataweza kujificha daima. Tutawakamata!.
4.
Mheshimiwa Spika, asubuhi ya tarehe 6 Mei,
2017, nchi yetu iliamka na simanzi kubwa kufuatia ajali iliyogharimu maisha ya
watu 36, wakiwemo wanafunzi 33, walimu wawili na dereva wao, waliokuwa kwenye
safari ya kimasomo Wilayani Karatu. Ajali hiyo imezima ndoto za vijana hao na
kuacha vilio kwenye familia zao. Namuomba Mwenyezi Mungu azilaze mahali pema
Peponi roho za marehemu. Aidha, nawaomba wazazi, walezi, walimu na marafiki wa
watoto hao waendelee kumtumainia Mwenyezi Mungu kwa mtihani huo mkubwa
walioupata. Naendelea kutoa wito kwa vyombo vyote vinavyohusika na ukaguzi wa
vyombo vya moto vya usafiri kwa wanafunzi na abiria wafanye ukaguzi wa kina na
wa mara kwa mara ili kuliepusha Taifa na ajali zinazoweza kuzuilika.
5.
Mheshimiwa Spika, nchi yetu pia ilipata
pigo la kuondokewa na watumishi wawili wastaafu waliolitumikia Taifa hili kwa
umahiri na uadilifu mkubwa. Watumishi hao ni marehemu Paul Sozigwa, aliyekuwa
Katibu wa Rais wa Awamu ya Kwanza; na Marehemu Said Mwambungu, aliyekuwa Mkuu
wa Mkoa wa Ruvuma. Namwomba Mwenyezi Mungu
awape pumziko la amani marehemu wote baada ya kulitumikia Taifa letu kwa
utumishi uliotukuka na umahiri mkubwa.
SHUGHULI ZA BUNGE
6.
Mheshimiwa
Spika, katika Mkutano huu, Bunge lako Tukufu limejadili na kupitisha bajeti za Wizara zote 19 na
Bajeti nzima ya Serikali Kuu, kupitisha Maazimio matano
(5) ya kuridhia Mikataba mbalimbali ya Kimataifa na kupitisha Miswada ya Sheria
mbalimbali, ambayo ni Muswada wa Sheria ya Fedha za Matumizi; Muswada wa Sheria
ya Fedha wa mwaka, 2017; Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali
wa Mwaka 2017; Muswada wa Sheria ya Mapitio na Majadiliano kuhusu Masharti Hasi
katika Mikataba inayohusu Maliasili za Nchi, 2017; na Muswada wa Sheria ya
Mamlaka ya Nchi kuhusiana na Umiliki wa Maliasili.
7.
Mheshimiwa
Spika, katika Mkutano huu jumla ya maswali 499 ya
msingi na mengine 1,834 ya nyongeza yaliulizwa na
Waheshimiwa Wabunge na kujibiwa na Serikali kupitia
kwa Waheshimiwa Mawaziri, Naibu Mawaziri na maswali ya papo kwa papo kwa Waziri
Mkuu. Vilevile, katika kipindi hiki Ofisi ya Bunge
iliendesha Semina mbalimbali kwa Waheshimiwa Wabunge kwa lengo la kuwajengea
uwezo zaidi na kuwapa uelewa mpana wa masuala mbalimbali yanayohusu maendeleo
ya nchi yetu.
8.
Mheshimiwa Spika, Bunge lako Tukufu pia
lilipata fursa ya kuchagua Wawakilishi wa Tanzania kwenye Bunge la Jumuiya ya
Afrika Mashariki, ambapo Wabunge tisa walichaguliwa. Kati ya Wabunge hao,
watano ni wanawake, na wanne ni wanaume. Ni matumaini yangu kuwa Waheshimiwa
Wabunge hao wataiwakilisha vema nchi yetu na kwamba watatimiza kikamilifu
wajibu wao kwa mujibu wa Mkataba wa Jumuiya ya Afrika Mashariki. Wizara ya
Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki inaelekezwa kufanya kazi kwa
karibu na Wabunge hao ikiwa ni pamoja na kuwapa ushirikiano unaostahili ili
waweze kutekeleza vizuri majukumu yao kwenye Bunge hilo.
9.
Mheshimiwa
Spika, nitumie fursa hii kukushukuru wewe binafsi
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Naibu Spika, Wenyeviti wa Bunge, Mwanasheria Mkuu wa Serikali na timu yake, Waheshimiwa
Mawaziri na Naibu Mawaziri, Waheshimiwa Wabunge na Watendaji na Wataalam wa Serikali pamoja na
watumishi wa Ofisi ya Bunge kwa kufanikisha kazi zote zilizopangwa kwenye Mkutano huu tena kwa ufanisi mkubwa.
10.
Ninawapongeza pia na
kuwashukuru Waheshimiwa Mawaziri na Naibu Mawaziri kwa maelezo mazuri ya
ufafanuzi waliyotoa wakati wa kujibu maswali mengi ya msingi na ya nyongeza ya
Waheshimiwa Wabunge pamoja na kujibu hoja za Kamati za Kudumu za Bunge na hoja
zilizotolewa na Waheshimiwa Wabunge binafsi ndani ya Bunge zima. Serikali
inathamini sana maoni na ushauri wa Waheshimiwa Wabunge, na tunaahidi kuendelea
kuzingatia maoni na ushauri wao.
AZIMIO
LA BUNGE KUUNGA MKONO JITIHADA ZA MHESHIMIWA RAIS
11.
Mheshimiwa
Spika, tarehe 14 Juni, 2017 Bunge lako Tukufu
lilipitisha Azimio la kumpongeza Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli;
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa hatua anazochukua kukabiliana na
upotevu wa mapato ya Serikali katika Sekta ya Madini. Aidha, tarehe 29 Juni,
2017 Bunge lako lilikubali kwa kauli moja kuridhia mabadiliko ya ratiba ya
Mkutano huu wa Bunge la Bajeti ili kuongeza siku tano za kazi kwa lengo la kuwezesha kujadili Miswada
mitatu ya mwaka 2017 inayohusu kulinda maliasili na rasilimali za Taifa ikiwemo
madini. Hii inadhihirisha kwamba Bunge hili ni la wananchi na linazingatia maslahi ya nchi.
12.
Mheshimwa
Spika, napenda kuungana na Waheshimiwa Wabunge
kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa uongozi wake
mahiri, juhudi na hatua stahiki anazoendelea kuchukua ili kuhakikisha kwamba
Watanzania na Taifa kwa ujumla wananufaika na rasilimali za Taifa. Nawasihi wananchi wote na viongozi, tuendelee kumuunga mkono Mheshimiwa Rais
katika jitihada zake hizo za kulinda maliasili za nchi
yetu.
HALI
YA ULINZI NA USALAMA:
13.
Mheshimiwa Spika, kwa ujumla hali ya ulinzi na usalama nchini ni shwari. Usalama wa raia na
mali zao unaendelea kulindwa, na mipaka yote ya nchi yetu iko salama. Aidha,
vikosi vya ulinzi na usalama viko imara na madhubuti katika kulinda mipaka na
usalama wa nchi yetu. Hata hivyo, wapo baadhi ya wenzetu wanaotishia usalama
wetu kwa kushiriki kwenye vitendo vya uhalifu wa kutumia silaha. Mathalan,
katika miezi ya hivi karibuni, kumekuwa na mauaji ya kuvizia katika maeneo ya
Mkuranga, Kibiti na Rufiji.
14.
Mheshimiwa Spika, dhamira ya Serikali ni kuhakikisha kuwa kila raia wa Tanzania, wakiwemo
wananchi wa Wilaya za Mkuranga, Kibiti na Rufiji wanakuwa huru kufanya shughuli
zao za maendeleo bila kuhofia usalama wa maisha yao. Serikali inaendelea
kuchukua hatua za muda mfupi na za muda mrefu ili kurejesha hali ya usalama
katika maeneo hayo. Tumeongeza doria na vitendea kazi kwa askari. Vilevile,
tumefanya maamuzi ya kuunda Kanda Maalum ya Kipolisi katika Mkoa wa Pwani
itakayojumuisha Wilaya za Mkuranga, Kibiti na Rufiji na tayari Kamanda wa
Polisi wa Kanda hiyo Maalum amekwishateuliwa. Hivyo, natoa wito kwa raia wema
katika Wilaya hizo, waendelee kutoa ushirikiano kwa Serikali ili kuwezesha
watuhumiwa wote kukamatwa.
15.
Mheshimiwa Spika, sanjari na mikakati ya kudhibiti uhalifu unaofanywa ndani ya nchi,
tunaendelea pia kudhibiti uhalifu unaovuka mipaka (cross border crimes). Ili
kutimiza jukumu hilo, tunaendelea kuboresha huduma za uhamiaji na kudhibiti
nyaraka zinazotolewa na Idara ya Uhamiaji. Tumeanzisha mfumo wa kuhakiki
nyaraka, hususan vibali vya kuishi nchini pamoja na Hati za Kusafiria.
Vilevile, tumehuisha utaratibu wa kisheria wa kutoa “migrant pass” kwa
wahamiaji walowezi, ili kuweza kuwatambua kwa urahisi. Kwa jitihada hizi,
tutaweza kudhibiti nyaraka za kughushi na kudhibiti wahalifu wa kimataifa
wanaovuka mipaka.
URATIBU WA MAAFA:
16.
Mheshimiwa Spika, katika msimu wa masika, baadhi ya maeneo ya nchi yetu yalipata mvua za juu
ya wastani na hivyo kusababisha maafa na madhara kwa wananchi ikiwemo vifo,
majeruhi na uharibifu mkubwa wa makazi na miundombinu. Mikoa iliyoathirika
zaidi ni Tanga, Arusha, Kagera, Dar es Salaam na visiwa vya Unguja na Pemba.
Kutokana na mvua hizo, watu 15 walipoteza maisha, 78 walijeruhiwa, nyumba 1,845
na majengo 36 ya taasisi mbalimbali yaliharibiwa katika viwango tofauti. Vilevile,
miundombinu ya barabara 48 katika mikoa 11 iliathiriwa na hivyo kuzorotesha kwa
muda usafiri na usafirishaji katika maeneo husika. Aidha, viwanja vya ndege vya
Arusha, Musoma, Ziwa Manyara, Mafia na Sumbawanga navyo viliathiriwa na mvua
hizo. Natoa pole kwa waathirika wote kutokana na kadhia hiyo.
17.
Mheshimiwa Spika, katika kukabiliana na athari za mvua hizo, Serikali iligharamia matibabu
ya majeruhi na mazishi ya waliopoteza maisha. Aidha, Serikali imetoa misaada ya
kibinadamu kama vile chakula, dawa, nguo na kufanya matengenezo ya dharura kwa
miundombinu iliyoharibika. Zoezi la ukarabati wa miundombinu iliyoharibiwa na
mvua linaendelea katika maeneo mbalimbali ya nchi.
18.
Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kutoa elimu kwa umma kuhusu menejimenti ya maafa
hususan kuzuia na kuweka mipango thabiti ya wananchi kujiandaa na maafa ili
kupunguza athari za maafa pindi yanapotokea. Aidha, tutaendelea kutoa taarifa
za utabiri wa hali ya hewa mara kwa mara na kwa wakati, ili kutoa fursa kwa
Mamlaka za Serikali za Mitaa na wananchi kujiandaa.
Vilevile, tutakamilisha mifumo ya ufuatiliaji wa maafa kwenye kituo chetu
cha Uratibu na Mawasiliano wakati wa Dharura; kuainisha na kutambua maeneo
hatarishi kwa maafa pamoja na kuendelea
kuijengea uwezo Idara yetu ya
Uratibu wa Maafa.
19.
Mheshimiwa
Spika, kuanzia tarehe
4 Aprili, 2017 hadi tarehe 20 Juni, 2017 Bunge
lako Tukufu lilipokea, kujadili na kupitisha Makadirio ya Mapato na Matumizi ya
Wizara, Taasisi mbalimbali za Umma, Mikoa, Mamlaka za Serikali za Mitaa pamoja
na Mfuko wa Bunge na Mfuko wa Mahakama. Aidha, Bunge lilipokea na kujadili Hoja
ya Serikali kuhusu Hali ya Uchumi wa Taifa kwa mwaka 2016, Mpango wa Maendeleo pamoja na makadirio ya Bajeti ya
Serikali ya Mwaka 2017/2018 ya jumla ya Shilingi Trilioni 31.7.
20.
Mheshimiwa Spika, niruhusu niungane na Waheshimiwa Wabunge wenzangu kumpongeza kwa dhati
Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango (Mb.), Waziri wa Fedha na Mipango na Naibu
Waziri, Mheshimiwa Dkt. Ashatu
Kijaji (Mb.) kwa hotuba nzuri ya Mpango wa Maendeleo
na Bajeti ya Serikali kwa mwaka 2017/2018. Nawapongeza
pia Watendaji wa Wizara ya Fedha na Mipango kwa umakini mkubwa wa maandalizi ya
Bajeti yenyewe. Aidha, nawapongeza kwa kutoa maelezo na ufafanuzi wa
kina kwa hoja za Waheshimiwa Wabunge wakati wa kuhitimisha Hoja hiyo. Kipekee
kabisa, nawapongeza na kuwashukuru
Waheshimiwa Wabunge kwa hoja za maboresho na kwa kupitisha Bajeti ya Serikali
kwa kura nyingi.
21.
Mheshimiwa Spika, kura za Waheshimiwa Wabunge kupitisha
Bajeti ya Mwaka 2017/2018 ni kielelezo kwamba, Bajeti hii inajibu kiu ya
wananchi ambao ninyi Waheshimiwa Wabunge mnawawakilisha. Kupitia michango yenu
na kwa pongezi zenu kwa Serikali, nimepata faraja kwamba mnathamini na
kuheshimu usikivu wa Serikali kwa maoni ya wananchi. Serikali hii ni sikivu,
makini na inazingatia maslahi ya wananchi walio wengi na hasa wa kipato cha
chini. Hivyo, napenda kulihakikishia Bunge
lako Tukufu kwamba, Serikali siyo tu itaendelea
kusikia, bali itasikiliza na kuchukua hatua, kama tulivyofanya kwenye Bajeti ya
mwaka 2017/2018 kwa kufuta kodi mbalimbali
za kero hasa katika kilimo na mifugo ili kuwawezesha wananchi kuongeza kipato
na kuboresha maisha yao.
22.
Mheshimiwa Spika, baada ya Bunge lako kuidhinisha Bajeti ya Serikali, tutahakikisha
tunasimamia utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo kwa Mwaka 2017/2018. Tayari
tumeandaa Mkakati wa Utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo, ambao unaainisha hatua
za utekelezaji, vigezo vya kupima ufanisi na hatua zinazotakiwa kuchukuliwa
katika kukamilisha miradi husika. Vilevile, tunaandaa mfumo wa kuhifadhi
taarifa za miradi ya maendeleo (National Project Databank) ili kufuatilia kwa
karibu utekelezaji wa miradi na changamoto zinazoikabili, kwa lengo la
kuikwamua. Sanjari na hatua hizo, Serikali imetoa maelekezo kwamba, Vitengo vya
Ufuatiliaji na Tathmini viimarishwe na kupewa nyenzo stahiki ili vifuatilie
miradi ya maendeleo hatua kwa hatua. Shabaha yetu ni kuhakikisha kuwa miradi
inasimamiwa kikamilifu, inaleta tija na kutekelezwa kwa ubora na viwango
vilivyoainishwa kwenye Mikataba.
23.
Mheshimiwa Spika,
ni ukweli usiopingika kwamba, mipango tuliyojiwekea haiwezi kufanikiwa, endapo
tutazembea katika ukusanyaji wa kodi na mapato ya Serikali. Hivyo, Serikali
itaendelea kubuni vyanzo vipya vya mapato;
kuimarisha ukusanyaji wa mapato; kudhibiti
biashara ya magendo; kuhimiza matumizi ya mashine za
kielektroniki katika ukusanyaji mapato na kudhibiti udanganyifu katika
ukadiriaji wa ushuru wa forodha. Wito
wangu kwa Waheshimiwa Wabunge ni kuhakikisha kuwa mnashirikiana na Halmashauri
kubuni vyanzo vya mapato na kuhamasisha ulipaji wa kodi bila shuruti.
24.
Mheshimiwa Spika, kulipa kodi ni uzalendo, tuwahamasishe wananchi wenzetu waone fahari
kuwa sehemu ya mafanikio ya nchi yetu kwa kulipa kodi na kuwafichua wakwepa
kodi. Ahadi yetu ni kuendelea kusimamia kila senti itakayokusanywa, ili
itekeleze jukumu lililokusudiwa. Aidha, tutaendelea kuimarisha usimamizi na
ufuatiliaji wa Bajeti iliyopitishwa na Bunge lako Tukufu ili kuhakikisha kwamba
fedha zilizotengwa zinatumika kwa umakini na kuleta
tija kwa maendeleo ya nchi yetu. Tulipe kodi kwa maendeleo ya nchi yetu!
SEKTA
YA KILIMO
Hali ya chakula
nchini
25.
Mheshimiwa Spika, napenda kuliarifu Bunge lako
Tukufu kwamba, hali ya chakula siyo ya
kuridhisha sana, bado kuna maeneo yenye upungufu wa
chakula. Pia, yapo maeneo yaliyopata mvua nyingi ambayo yamepata chakula cha
kutosha. Hii ni kutokana na mazao ya chakula katika maeneo hayo kuanza kukomaa. Aidha,
kutokana na wakulima katika baadhi ya maeneo kuanza kuvuna mazao yao, mwenendo
wa bei za vyakula hususan mahindi imeanza kushuka katika masoko mbalimbali.
Hata hivyo, kutokana na nchi zinazotuzunguka kuwa na upungufu mkubwa wa chakula, na
umuhimu wa kuwa na usalama na kujitosheleza kwa hifadhi ya chakula, ni vizuri
kila kaya ikahakikisha kwamba inakuwa na akiba ya chakula kwa matumizi ya
baadaye. Aidha, tumepiga marufuku usafirishaji mahindi nje ya nchi bila kibali,
badala yake tunahamasisha uongezaji wa thamani ya mazao badala ya kusafirisha
nafaka ghafi. Hii inatokana na kuwepo na maeneo ambayo hadi sasa hayana chakula
cha kutosha. Nashauri Wafanyabiashara wasambaze mahindi huko. Aidha, natoa wito
kwa Wakuu wa Mikoa ya Mipakani kutekeleza agizo la Serikali la kuchukua hatua
kwa watakaokiuka agizo hilo.
Mfumo mpya wa
Usambazaji wa Mbolea
26.
Mheshimiwa
Spika, Serikali inajipanga vyema
msimu ujao wa kilimo kwa kusambaza pembejeo na kuhamasisha matumizi ya mbolea.
ili kufanikisha azma hiyo, katika bajeti ya Mwaka 2017/18 Serikali
imeamua kuimarisha utaratibu wa upatikanaji na usambazaji mbolea kupitia Mfumo
wa Uagizaji wa Mbolea kwa Pamoja (Fertilizer
Bulk Procurement System).
27.
Mheshimiwa
Spika, kupitia mfumo huo, mbolea itaagizwa na waagizaji
watakaopitishwa kwenye utaratibu wa zabuni,
na wakulima wataweza kununua mbolea hiyo katika maduka ya pembejeo vijijini
kwa bei dira itakayopangwa na Serikali. Mfumo huo mpya utaanza kwa kuingiza
mbolea ya kupandia aina ya DAP na mbolea ya kukuzia aina ya UREA ambazo
zinatumiwa na wakulima wengi. Mbolea za aina nyingine zitaendelea kuletwa kwa
utaratibu wa zamani. Napenda kurejea maelekezo yangu kwa Wizara ya Kilimo,
Mifugo na Uvuvi kwamba isimamie kikamilifu zoezi hili la usambazaji wa mbolea
ili kuhakikisha kuwa mbolea inawafikia wakulima miezi miwili au mitatu kabla ya
msimu wa kilimo haujaanza.
Maboresho
kwenye Sekta ya Mifugo
28.
Mheshimiwa
Spika, pamoja na idadi kubwa ya mifugo tuliyonayo
nchini, lakini mchango wake kwenye Pato la Taifa na katika kutuingizia fedha za
kigeni siyo wa kuridhisha. Kutokana na hali
hiyo, tarehe 15 Juni 2017 nilikutana na Maafisa Mifugo wa Wilaya zote nchini
kwa lengo la kuweka mikakati ya pamoja ya kuboresha sekta ya mifugo nchini ili
iweze kuleta tija na kuongeza mchango wake kwenye Pato la Taifa. Miongoni mwa mikakati tuliyojiwekea ni pamoja na kuwawezesha wafugaji kupata maeneo mahsusi ya malisho ya
mifugo yao na kuwapatia mafunzo ya stadi za ufugaji bora. Vilevile, tumetoa
maelekezo kwa Maafisa Mifugo kuwatembelea wafugaji ili kuwahudumia na kuwapa
mafunzo ya ufugaji bora. Aidha, tumezindua Mwongozo wa Ufugaji Bora nchini,
ambao utakuwa ni dira ya kuwaongoza wafugaji kuhusu namna ya kuboresha sekta ya
mifugo nchini. Lengo letu ni kuwa na mifugo michache lakini yenye tija kubwa.
Hata hivyo, tumekemea wafugaji wasilishe mifugo yao katika mashamba yenye mazao
ya chakula, na pia kuchungia kwenye misitu iliyohifadhiwa. Hatua kali
zitachukuliwa dhidi ya watakaokiuka agizo au katazo hilo.
SEKTA
YA ARDHI
Upimaji na Umiliki wa ardhi
29.
Mheshimiwa
Spika, ardhi isiyopimwa ina thamani ndogo na ni chanzo
cha migogoro isiyo ya lazima. CCM iliona jambo hili, na kupitia Ilani ya
Uchaguzi ya mwaka 2015, iliielekeza Serikali kuhakikisha kuwa kila kipande cha
ardhi ya Tanzania kinapimwa. Napenda kuliarifu Bunge lako Tukufu kwamba,
Serikali imeweka Mkakati na Mpango Kazi wa kuwezesha kufikia lengo la kupanga
matumizi bora ya ardhi katika vijiji 1,500 na
wilaya 5 kila mwaka. Aidha, Serikali inaendelea kuchukua hatua stahiki za kupunguza gharama za umilikaji wa ardhi nchini.
Katika Mwaka wa Fedha 2017/2018, Serikali imepunguza tozo ya mbele (premium)
kutoka asilimia 7.5 ya thamani ya ardhi hadi asilimia 2.5 tu. Natoa wito kwa
wananchi kuchangamkia punguzo hili na kujitokeza kupimiwa na kumilikishwa
ardhi.
Kuimarisha Huduma katika Ofisi za Ardhi za Kanda
30.
Mheshimiwa
Spika, kazi ya upimaji wa ardhi haiwezi kufanikiwa bila
ya rasilimali watu. Serikali itaendelea kuimarisha Ofisi za Ardhi za Kanda kwa
kupeleka wataalam wa kada mbalimbali na kuwawezesha kwa kuwapatia vitendea kazi
stahiki. Lengo letu ni kuwawezesha wananchi kupata huduma mbalimbali za ardhi
katika kanda badala ya kufuata huduma hizo Makao Makuu ya Wizara. Nawasihi
watumishi watakaohamishiwa katika Ofisi za kanda pamoja na wale waliopo katika
Halmashauri, wafanye kazi kwa ushirikiano na watekeleze majukumu yao kwa
kuzingatia sheria, kanuni na
taratibu zinazosimamia sekta ya ardhi na kutoa huduma kwa wananchi bila ubaguzi, bila usumbufu na bila ya kuomba rushwa ya aina yoyote ile.
SEKTA YA WANYAMAPORI
Hifadhi
ya Mapori
31.
Mheshimiwa Spika, asilimia
28 ya eneo la nchi yetu limetengwa kwa ajili ya kuhifadhi rasilimali za Taifa
ikiwemo misitu, wanyamapori, na utunzaji mazingira kwa ajili ya matumizi ya
binadamu na viumbe hai wakiwemo wanyamapori ambao wanachangia kwa kiwango
kikubwa katika shughuli za utalii. Changamoto kubwa iliyopo sasa katika mapori
yetu ya hifadhi ni uvamizi wa mifugo, na kwa bahati mbaya kwenye mikoa ya
mipakani, mifugo mingi imekuwa inatoka nchi jirani.
32.
Ili kuhakikisha kwamba
Hifadhi za Taifa na mbuga zetu za wanyamapori zinalindwa kikamilifu. Mwezi
Novemba, 2016 niliagiza Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kushirikiana na Ofisi
ya Rais TAMISEMI na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kuweka alama
za mipaka (beacons) kuainisha maeneo
yote ya hifadhi nchini kwa lengo la kuondoa migogoro iliyopo. Baada ya kuweka
alama hizo, Serikali imeanza rasmi zoezi la kuondoa mifugo yote ndani ya
hifadhi. Aidha, nimeelekeza kwamba, uwekaji wa alama au nguzo hizo uhusishe
Halmashauri za Wilaya na Ofisi za Wakuu wa Wilaya. Ramani zinazoonyesha mapori
zitumike. Aidha, mapori yote yaliyohifadhiwa kisheria yaheshimike.
33.
Mheshimiwa Spika, kufuatia kuwepo kwa migogoro baina ya Wafugaji na Wakulima na migogoro
baina ya wafugaji na wahifadhi wa mapori, nimeelekeza kwamba ifikapo mwisho wa
mwezi Julai 2017 Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi wabainishe maeneo yote ya
Ranchi za Taifa za Mifugo ambazo hazitumiki na kuzigawa katika vitalu (blocks) kwa wafugaji ili mifugo mingi
iondolewe vijijini na ipelekwe kwenye maeneo hayo ili Serikali iweze kutoa
huduma za ugani za kisasa huko kwenye hizo blocks.
34.
Natoa wito kwa wafugaji
wote nchini kufuata Sheria za Hifadhi za Taifa, Mbuga za Wanyamapori, maeneo
tengefu pamoja na vyanzo vya maji. Mifugo yote itakayokutwa ndani ya hifadhi,
hatua kali zitachukuliwa na kufikishwa mahakamani. Aidha, tukumbuke kuwa ardhi
haiongezeki lakini wafugaji na mifugo vinaongezeka, hivyo ni lazima tufuge
kisasa na tufuge mifugo michache yenye tija ambayo tutaweza kuihudumia katika
maeneo yatakayotengwa kwa ajili ya ufugaji.
SEKTA YA AFYA
Ununuzi wa dawa na vifaa tiba
35.
Mheshimiwa
Spika; kama ambavyo
nimekuwa nikisisitiza kuhusu umuhimu wa afya bora kwa wananchi wetu, Serikali itaendelea kutoa kipaumbele katika kuboresha
upatikanaji wa dawa na vifaa tiba kwa kununua,
kutunza na kusambaza dawa, vifaa tiba na vitendanishi katika vituo vya kutolea huduma
za afya nchini. Katika mwaka wa fedha 2017/2018, Serikali
imetenga jumla ya Shilingi bilioni 236 zikiwa ni fedha za ndani kwa ajili
hiyo. Aidha, Serikali imetenga fedha za ndani kiasi cha Shilingi Bilioni
33 kwa ajili ya chanjo za watoto na makundi maalum. Nitoe rai kwa
wazazi/walezi kuhakikisha watoto wao wanapata chanjo zote zinazotakiwa ili
kuwakinga na magonjwa na kuwajengea msingi mzuri wa maisha yao ya baadaye. Aidha, kila mwananchi
ajenge utamaduni wa kupima afya yake mapema ili kubaini
tatizo lake la kiafya mapema, badala ya kusubiri hadi ugonjwa ufike hatua mbaya ndipo aende hospitali.
Vifo vitokanavyo na
uzazi
36.
Mheshimiwa Spika, tatizo la vifo vitokanavyo na
uzazi bado ni changamoto kubwa katika nchi yetu. Takwimu za hivi karibuni
zinaonesha kuwa idadi ya vifo vitokanavyo na uzazi ni 556 kwa kila vizazi hai 100,000.
Hali hii haikubaliki na haivumiliki, kwani wanaopoteza maisha ni Watanzania
wenzetu, ni mama zetu, ni wake zetu, ni dada zetu na ni watoto wetu. Tumesikia
maoni na michango ya Waheshimiwa Wabunge kuhusu suala hili wakati wa Mjadala wa
Bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu, bajeti ya Wizara ya Afya na Bajeti ya Serikali
iliyowasilishwa na Waziri wa Fedha na Mipango.
37.
Napenda
kulihakikishia Bunge lako Tukufu kwamba, Serikali imewasikia na kwa hakika inaguswa sana na vifo vitokanavyo na
uzazi. Ndio maana Serikali imeamua kuongeza fedha za ndani kwa ajili ya kuimarisha huduma
za Afya ya Mama na Uzazi. Serikali imeamua kwamba, itanunua,
kusambaza na kutoa bila malipo dawa
kwa ajili ya uzazi salama katika vituo vya umma vya kutolea huduma. Hii ni pamoja na dawa ya kuzuia kutokwa na damu baada ya kujifungua, dawa kwa ajili ya
kifafa cha mimba na dawa kwa ajili ya kuongeza damu. Jumla ya shilingi bilioni 7 zimetengwa kwa ajili ya kazi hiyo. Vilevile, Serikali imejizatiti kuongeza kasi ya
ujenzi wa vituo vya afya na zahanati vijijini pamoja na kuimarisha vituo vyote
vya kutolea tiba nchini kwa lengo la kuboresha huduma za Afya. Hivyo, napenda
kuwahakikishia wanawake wote nchini, kwamba hakuna mwanamke mjamzito atakayepoteza maisha kwa kukosa dawa/sindano
ya kuzuia kuvuja damu au kukosa dawa ya kuzuia kifafa cha mimba.
SEKTA YA ELIMU
Kuinua Ubora wa Elimu na Mafunzo
38.
Mheshimiwa
Spika, kwenye hotuba yangu ya
kufungua mkutano
wa saba wa Bunge lako tukufu, unaoahirishwa leo nilieleza kwa kirefu umuhimu wa watoto wetu kutoa
kipaumbele kwa masomo ya sayansi. Nilisema, endapo watoto wetu hawatasoma
masomo ya sayansi, watabaki kuwa watazamaji kwenye uchumi wa viwanda. Napenda
kuliarifu Bunge lako tukufu, kwamba,
Serikali imeanza kutimiza wajibu katika kuweka mazingira wezeshi kwa watoto
wetu kujifunza masomo ya sayansi kwa
vitendo.
39.
Tarehe 6 Juni, 2017 nilizindua zoezi la usambazaji wa vifaa vya maabara kwa ajili ya shule za sekondari 1,696 vyenye thamani ya shilingi bilioni
16.9. Vifaa hivyo
vinaendelea kusambazwa katika shule za Tanzania Bara ambazo zimekamilisha
ujenzi wa maabara. Hivyo, natoa wito kwa wanafunzi kutumia vifaa hivyo kusoma
kwa bidii masomo ya sayansi, na kuvitunza ili vinufaishe wanafunzi wengi zaidi.
Aidha, Halmashauri zote nchini ambazo
hazijakamilisha ujenzi wa maabara
zinaelekezwa kukamilisha zoezi hilo mapema, ili vifaa vingine vitakapoletwa
visambazwe haraka.
Elimu Jumuishi
40.
Mheshimiwa
Spika, sambamba na jitihada za
kuinua ubora wa elimu nchini, Serikali imeendelea kutafuta suluhu ya changamoto
za kujifunzia zinazowakabili wanafunzi wenye mahitaji maalum. Hivi karibuni
Serikali imenunua vifaa kwa ajili ya wanafunzi wasioona na wenye baki ya
usikivu na kuvisambaza katika shule 213
za msingi na 22 za sekondari. Aidha, Serikali imenunua vifaa vya upimaji ili kubaini watoto
wenye mahitaji maalum ya ujifunzaji kwa mikoa yote
Tanzania Bara. Rai yangu kwa wazazi wenzangu kote nchini, ni kutumia fursa hii
kuwapeleka shuleni watoto wenye mahitaji maalum badala ya kuwaficha majumbani.
Shabaha ya Serikali ni kuhakikisha kuwa kila
mtoto wa Tanzania mwenye umri wa kwenda shule, anapata fursa hiyo bila kujali uwezo wake wa kifedha au changamoto za kimwili.
Msimamo wa Serikali kuhusu Ujauzito shuleni
41.
Mheshimiwa
Spika, moja kati ya mijadala iliyoibua hisia kali wakati
wa mjadala wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ni pamoja na kuwaachisha masomo wanafunzi waliopata ujauzito
shuleni. Kwa mujibu wa takwimu za mwaka 2015, jumla ya wanafunzi 3,637 waliacha masomo kutokana na
kupata ujauzito. Kuwaachisha masomo wanafunzi waliopata ujauzito, ni
utekelezaji wa Waraka na Kanuni za Elimu
za Mwaka 2002 zinazohusu kufukuza na kuondoa wanafunzi shuleni kutokana na
makosa mbalimbali ikiwemo uasherati, wizi, ulevi, kutumia
dawa za kulevya pamoja na utoro unaotokana na baadhi ya wanafunzi kwenda
kufanya shughuli za biashara ndogo ndogo, kucheza kamali, kuvua samaki,
kuchimba madini, n.k.
42.
Mheshimiwa Spika, msimamo wa Serikali wa kutoruhusu wanafunzi waliopata ujauzito
kuendelea na masomo katika mfumo rasmi wa elimu ni kwa mujibu wa sheria na wala
sio utaratibu mpya kama inavyopotoshwa na baadhi ya wanaharakati. Msimamo huo
wa kisheria unalenga kuwafanya watoto wa kike wajishughulishe na masomo yao
badala ya kushiriki kwenye vitendo vya ukiukwaji wa maadili. Lengo hili pia nalo
ni la kuwaelimisha wazazi kila mmoja aendelee kumtunza binti yake na kuwafundishe
watoto wao mambo mema na maadili mema ndani ya familia. Wazazi wajishughulishe
kikamilifu katika kuweka katazo kwa watoto kujihusisha na ngono wakiwa na umri
mdogo. Dhamira ya Serikali ni kumlinda mtoto wa kike ili apate elimu kwa ajili
ya manufaa yake na Taifa kwa ujumla. Sote tutakumbuka kaulimbiu ya mke wa Rais
wa awamu ya nne, Mama Salma Rashid Kikwete aliyesema: “Mtoto wa mwenzio ni
mwanao.” Kila mzazi hana budi kujikita kuwalea watoto hawa badala ya
kuwafanyisha vitendo ambavyo havistahili.
43.
Mheshimiwa Spika, kila Mtanzania ana wajibu wa kuhakikisha kuwa watoto wetu wanapata
elimu. Hivyo, ni lazima tuhakikishe mtoto wa kike anapata elimu stahiki na
masomo yake hayakatizwi kwa kupata ujauzito. Serikali imewekeza kwenye mtoto wa
kike. Kifungu Na. 60 (b) cha Sheria ya Elimu Sura ya 353, kinatoa adhabu ya
miaka 30 jela kwa yeyote atakayeoa au kumpa ujauzito mwanafunzi. Aidha, sheria
inatoa adhabu ya kifungo cha miaka mitano jela au faini ya Shilingi Milioni 5, au vyote kwa pamoja kwa anayeshiriki kumuozesha
mtoto wa shule. Natoa wito kwa Wakuu wa Wilaya kusimamia utekelezaji wa sheria
za nchi zenye lengo la kumlinda mtoto wa kike. Aidha, nawashauri Waheshimiwa
Wabunge, mshirikiane na Halmashauri zenu kuweka mikakati ya kudhibiti ujauzito
kwa watoto wa shule. Wahamasisheni wananchi watoe ushirikiano kwa vyombo vya
dola, ili wanaowapa wanafunzi ujauzito au kuwakatisha masomo ili waozeshwe
wapate adhabu stahiki.
SEKTA YA MAJI
44.
Mheshimiwa
Spika, katika mjadala wa Bajeti moja ya sekta ambayo Waheshimiwa Wabunge wengi walionesha kwamba inahitaji
kupewa kipaumbele cha pekee ni sekta ya maji. Hakika nakubaliana na mtazamo huo
wa Waheshimiwa Wabunge kwani maji ni uhai na kichocheo cha maendeleo katika sekta mbalimbali na nyenzo muhimu katika mapambano dhidi ya umaskini. Kwa
kuwa suala la maji lilitolewa ufafanuzi wa kina na Mheshimiwa Waziri wa Maji na
Umwagiliaji na Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Mipango, naomba Waheshimiwa Wabunge
watuelewe kwamba tumewasikiliza na tumewasikia. Serikali
inayo nia ya dhati kuhakikisha kwamba vijiji zaidi vinapata huduma ya maji.
UBORESHAJI WA MAMLAKA ZA SERIKALI ZA MITAA NCHINI
45.
Mheshimiwa
Spika, Serikali imeendelea kuchukua hatua madhubuti katika
kuhakikisha kuwa Mamlaka za Serikali za Mitaa nchini
zinatimiza malengo ya kuanzishwa kwake kwa mujibu wa Ibara ya 145 na 146 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, 1977. Miongoni mwa hatua zinazochukuliwa na
Serikali ni pamoja na kuendeleza juhudi za ugatuaji wa madaraka kwenda katika
vyombo hivyo pamoja na kuongeza mgawo wa fedha za ruzuku ya maendeleo
inayopelekwa katika Mamlaka za Serikali za Mitaa.
46.
Mheshimiwa
Spika, katika kutekeleza azma hiyo, Serikali katika mwaka 2017/2018 imetenga kiasi cha shilingi bilioni 412.38 kwa ajili ya miradi ya maendeleo.
Kati ya fedha hizo:-
(i)
Serikali imetenga jumla ya shilingi bilioni 16.985 kwa ajili ya kuboresha
miundombinu ya majengo ya Ofisi na Makazi ya Viongozi katika Mikoa yote mipya.
Katika mgawo huo, Mkoa wa Njombe umetengewa jumla ya shilingi bilioni 3.34; Mkoa wa Katavi umetengewa
jumla ya shilingi bilioni 3.080;
Mkoa wa Simiyu umetengewa jumla ya Shilingi Bilioni 3.775, Mkoa wa Geita umetengewa jumla ya shilingi bilioni 2.978 na Mkoa wa Songwe
umetengewa jumla shilingi bilioni 3.812.
(ii)
Aidha, Serikali imetenga jumla ya shilingi
bilioni 61.7 kwa ajili ya ujenzi wa
Makao Makuu ya Halmashauri 64, Kati
ya fedha hizo, shilingi bilioni 28.7
ni kwa ajili ya kukamilisha majengo ya Ofisi katika Halmashauri 44 na shilingi
bilioni 33 ni kwa ajili ya ujenzi wa
Makao Makuu ya Halmashauri mpya 20.
Kwa sasa
Serikali haina mpango wa kuanzisha maeneo mapya ya utawala mpaka tukamilishe
maeneo tuliyoyaanzisha kwa kuboresha miundombinu.
(iii)
Sambamba na hatua hizo, Serikali
kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Wazee na Watoto imetoa vifaa
mbalimbali kwa ajili ya kuboresha huduma za afya katika Mamlaka za Serikali za
Mitaa vyenye thamani ya shilingi bilioni
2.9 pamoja na kununua magari ya kubebea wagonjwa katika Halmashauri 67.
(iv)
Vilevile, Serikali imeandaa mpango
mahsusi wa kuwajengea uwezo
Wakurugenzi wa Halmashauri pamoja na Watendaji wa Kata, Vijiji, Mitaa na
Vitongoji ili waweze kutoa huduma bora na kwa ufanisi katika kuwahudumia
wananchi. Sehemu ya fedha za maendeleo zitatumika kwa ajili ya kujenga uwezo wa
watendaji wa Mamlaka za Serikali za Mitaa.
47.
Mheshimiwa
Spika, juhudi za Serikali za kuimarisha utendaji wa
Mamlaka za Serikali za Mitaa zina lengo la kusogeza huduma karibu na wananchi
na kutatua kero zao katika ngazi hiyo. Aidha, jitihada hizo zimelenga kuongeza
kasi ya maendeleo Vijijini na kuboresha maisha na ustawi wa wananchi wetu. Kwa
msingi huo, natoa wito kwa Viongozi wa Mikoa na Wilaya
pamoja na Halmashauri, wahakikishe kwamba malalamiko yote ya wananchi
yanatatuliwa haraka katika ngazi husika. Si vyema na haikubaliki kwa wananchi
kusafiri umbali mrefu kutafuta suluhu za changamoto zao kwa viongozi wa Kitaifa
wakati wa Mamlaka za Serikali za Mitaa zipo, na zina Viongozi wanaolipwa mishahara kwa fedha za walipa kodi.
Serikali itaendelea kufuatilia utekelezaji wa maagizo yanayotolewa kuhusu suala
hili.
MAPAMBANO DHIDI YA DAWA ZA KULEVYA
48.
Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea na mapambano dhidi ya uzalishaji, uuzaji,
usambazaji na utumiaji wa dawa za kulevya nchini. Tumeendelea kubaini mtandao
wa waingizaji wa dawa hizo hapa nchini na kuchukua hatua stahiki dhidi ya
wahalifu hao. Ili kuimarisha mapambano hayo na kuyaendesha kisayansi, Serikali
imekamilisha uteuzi wa watendaji mahiri wa Mamlaka ya Kupambana na Dawa za
Kulevya wanaojumuisha makamishna wanne waliobobea kwenye taaluma zao na wenye
uzalendo na uzoefu mkubwa kwenye mapambano haya.
49.
Mheshimiwa Spika, Katika kipindi kifupi tangu mwezi Februari, 2017 Mamlaka hii
ilipozinduliwa, imefanikiwa kukamata watuhumiwa 4,809 wakiwa na dawa za kulevya aina ya heroine (gramu 327.173); cocaine (kilo 26.977); bhangi (kilo 18,334.83); mirungi (kilo 11,306.67) na lita 6,338 za kemikali bashirifu zilikamatwa bandarini. Aidha,
Mamlaka kwa kushirikiana na Kamati za Ulinzi za Mikoa imefanya operesheni za
kuteketeza ekari 569.25 za mashamba ya bhangi na ekari 64.5 za mashamba ya mirungi na
kazi hiyo inaendelea. Kutokana na hatua hizo, jumla ya majalada ya kesi 3,222 yamefunguliwa.
50.
Mheshimiwa Spika, dawa za kulevya zina athari kubwa kwa ustawi wa familia zetu na Taifa
kwa ujumla. Hivyo, napenda kurejea wito wangu kwa Watanzania wote kuunga mkono
jitihada za Serikali katika mapambano haya kwa kuendelea kutoa taarifa kuhusu
watu wote wanaojihusisha na biashara ya dawa za kulevya. Aidha, naendelea kutoa
rai kwa wazazi wenzangu kufuatilia mienendo ya watoto wetu ili wasijiunge
katika makundi mabaya ya kujihusisha na dawa za kulevya. Itakumbukwa kwamba
waathirika wakubwa wa dawa za kulevya ni vijana wenye umri kati ya miaka 15-35,
kundi ambalo ni tegemeo kwa ustawi wa Taifa letu.
51.
Mheshimiwa Spika, Azma ya Serikali ya awamu ya tano ni kutokomeza kabisa mtandao wa dawa
za kulevya nchini kwa kuhakikisha kuwa mapambano dhidi ya dawa za kulevya
yanakuwa endelevu, yanafanyika kisayansi na yanaleta mafanikio. Tuungeni mkono
kwenye mapambano haya, ili itokomeze kabisa mtandao huo.
SEKTA YA MICHEZO
52.
Mheshimiwa
Spika, wakati vikao vya Bunge hili vikiendelea, tmu yetu ya vijana walio chini ya umri wa miaka 17, Serengeti Boys ilishiriki na kutoa upinzani mkubwa kwenye
mashindano ya Shirikisho la Mpira wa Miguu
Barani Afrika ambapo ilimaliza ikiwa na jumla ya pointi 4 sawa na timu iliyoshika nafasi ya pili. Hata hivyo, kutokana na kanuni
za mashindano hayo, Serengeti Boys haikuweza kuendelea
na mashindano pamoja na matokeo hayo mazuri.
53.
Mheshimiwa
Spika, binafsi nilifuatilia mechi zote za Serengeti Boys
nikiri kwamba, vijana hao wana vipaji na uzalendo wa hali ya juu kwa nchi
yao. Kwangu mimi vijana wale ni washindi bila hata ya kupewa taji lolote. Naomba nitumie Bunge lako tukufu,
kuwapongeza kwa dhati kudhihirisha kwamba hakuna
linaloshindikana tukiamua. Msisitizo wangu kwa TFF
ni kuendelea kuwatunza
vijana hao, na kusimamia vilabu vya
michezo nchini kuwekeza kwenye soka la vijana ili tujenge timu imara kwa miaka
michache ijayo.
54.
Mheshimiwa
Spika, Serikali inatambua umuhimu wa michezo kwa afya,
umoja wa kitaifa na kama fursa ya ajira kwa vijana wetu. Wiki iliyopita, mkoani Mwanza yamehitimishwa
mashindano ya UMISSETA na UMITASHUMTA. Wananchi wa
Mwanza na Watanzania kwa ujumla wamejionea uwezo wa kimichezo, vipaji na hamasa kubwa iliyopo miongoni mwa vijana wetu kutumia vipaji vyao. Hivyo, tutaendelea kuratibu michezo shuleni, ikiwa ni pamoja na kusimamia ufundishaji wa
michezo kama somo. Maelekezo yetu ni kwamba kila Mkoa uwe na shule angalau
mbili zenye mchepuo wa michezo na walimu wenye sifa stahiki za kufundisha
michezo. Nawapongeza sana Walimu wetu kwa kusimamia vizuri michezo shuleni.
Nitumie fursa hii kuagiza Wakurugenzi wa Halmashauri zote nchini, wahakikishe
kwamba kila shule inakuwa na viwanja vya michezo mbalimbali ili kuwapa fursa
wanafunzi kushiriki michezo ili kupandisha na kuinua vipaji vyao, na walimu
wanahimizwa wasimamie michezo mbalimbali shuleni.
55.
Mheshimiwa
Spika, naomba nitumie fursa hii kuwashukuru wadhamini
waliodhamini michezo yetu ya UMITASHUMTA na UMISSETA mwaka huu wa 2017 ambao ni
Coca Cola, LAPF na Chama cha Walimu Tanzania (CWT) kwa mchango wao mkubwa.
56.
Mheshimiwa
Spika, nitumie fursa
hii kumpongeza Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuunga mkono jitihada za
michezo nchini kwa dhamira yake ya kujenga uwanja mkubwa wa michezo hapa mjini Dodoma kwa kushawishi mataifa rafiki
kama vile Morocco ambao wanajenga uwanja huo.
Serikali ya
Awamu ya Tano itaendelea kusimamia michezo nchini na haitafumbia
macho usimamizi mbovu, na utawala wa michezo usiojali maslahi ya Taifa. Serikali imeazimia kuimarisha utendaji kwa vyombo
vya michezo nchini ili kila mwenye dhamana awajibike ipasavyo. Kwa msingi huo, leo hii naelekeza kwa Waziri mwenye dhamana ya michezo nchini
kulifanyia mapitio na kutathmini upya Baraza la Michezo Tanzania (BMT) ili kujiridhisha na usimamizi wake wa shughuli za michezo
nchini. Pale itakapodhirika kwamba usimamizi siyo imara, anayo ruhusa ya
kulivunja Baraza hilo na kuunda Baraza jipya.
HITIMISHO
57.
Mheshimiwa Spika, kabla ya kuhitimisha hotuba yangu, naomba nirejee masuala makubwa
niliyoyasisitiza wakati nafungua Mkutano wa Saba wa Bunge lako tukufu. Masuala
hayo niliyoyasisitiza, ambayo naamini bado yana umuhimu hadi sasa kwa ustawi wa
nchi yetu ni kama ifuatavyo:-
(i)
Moja, tuendelee kulinda na kudumisha amani nchini
ili wananchi washiriki shughuli za maendeleo bila hofu ya usalama wao.
(ii)
Pili, jukumu la kujenga uchumi wa nchi yetu ni wajibu
wa kila mwananchi. Ni lazima kila mwananchi afanye kazi kwa bidii na maarifa, alipe kodi stahiki na afichue wanaokwepa kulipa kodi.
(iii) Tatu, tujenge utamaduni wa kupima afya zetu na kufanya
mazoezi ya viungo ili kujilinda na
magonjwa yasiyo ya kuambukiza ambayo yanaigharimu sana nchi
yetu;
(iv)
Nne, tuepuke matumizi mabaya ya rasilimali zetu kama vile maji, madini na misitu ili
zinufaishe kizazi chetu na vizazi vijavyo;
(v)
Tano, tuzingatie matumizi ya muda, tuongeze
nidhamu na uwajibikaji tuzingatie muda na kupiga
vita tamaduni zote zinazohamasisha uvivu na uzembe; na
(vi)
Mwisho, dawa za kulevya ni janga kubwa linaloitafuna
kwa kasi nguvukazi ya nchi yetu. Tunahitaji ushiriki wa kila mmoja katika vita
hii kwa kufichua mtandao wa wahusika wa dawa za kulevya.
58.
Mheshimiwa
Spika, nihitimishe hotuba yangu,
kwa kuwatakia safari njema Waheshimiwa
Wabunge wanaporejea majimboni kuwaeleza wananchi mambo mengi yaliyojiri hapa Bungeni hususan kuhusu
manufaa ya Bajeti na miswada tuliyoipitisha. Waelezeni
wananchi matarajio yetu kwao na kuwasihi waendelee kutuunga mkono kwenye
jitihada zetu za kuwawekea mazingira wezeshi ya kujikwamua na umaskini.
Serikali inaendelea kusisitiza ushirikiano baina ya Waheshimiwa Wabunge na
Halmashauri zenu, katika ufuatiliaji wa fedha za maendeleo tunazoleta kwenye
Halmashauri, ili zifanye kazi iliyokusudiwa. Aidha, naitakia maandalizi mema
Timu yetu ya Bunge itakayoshiriki kwenye mashindano ya Mabunge ya Jumuiya ya Afrika
Mashariki yatakayofanyika mwaka huu mjini Dodoma. Tunayo imani kubwa na Timu
yetu, tuwakilisheni vizuri, kama ilivyo kawaida.
59.
Mheshimiwa
Spika, baada ya maelezo hayo, napenda kutoa hoja kuwa
Bunge lako Tukufu liahirishwe hadi tarehe 05 Septemba, 2017 siku ya Jumanne, Saa 3:00 asubuhi litakapokutana
katika ukumbi huu hapa Dodoma.
60.
Mheshimiwa
Spika, naomba kutoa hoja.
COMMENTS