Tarehe 9 Julai, 2017, magazeti ya The Guardian na The Citizen yaliandika habari  kuhusu Kampuni ya MANTRA Tanzania kusitisha (Suspension) uchimbaji wa Madini ya Urani (Uranium) kwenye leseni yao iliyoko eneo la Mto Mkuju sababu zikiwa ni
kuporomoka kwa bei ya Urani katika Soko la Dunia pamoja na mabadiliko katika Sheria ya Madini.

Ieleweke kuwa, Kampuni ya Mantra Tanzania inayo leseni ya Uchimbaji Mkubwa wa Madini (Special Mining Licence) SML NO. 489/2013 yenye eneo la ukubwa wa kilometa za mraba 197.94 iliyotolewa tarehe 05/04/2013 na kabla ya Kampuni hiyo kuomba leseni ya uchimbaji madini ilifanya upembuzi yakinifu (feasibility study) na kuthibitisha kuwa kwa bei ya Urani ya wakati huo ambayo ilikuwa ni Dola za Marekani 65 kwa Ratili moja (US$ 65/Pound) hivyo mradi huo ungezalisha madini kwa faida.  

Hata hivyo, bei ya Urani duniani ilianza kuporomoka na kufikia Dola 18.5 kwa ratili mwanzoni mwa mwaka 2017 na kwa sasa bei ni Dola 23 kwa ratili moja. Kufuatia kuporomoka huko kwa bei, Kampuni ilikokotoa gharama na kuonekana kuwa haiwezi kuzalisha urani kwa faida. 

Tarehe 14/12/2016, Kampuni ilimuandikia Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini ikiomba Waziri mwenye dhamana na Madini atoe ridhaa (consent) ili wasitishe uchimbaji kwa muda wa miaka mitano kwa ajili ya kuangalia kama bei inaweza kupanda ndipo waanze uchimbaji.  Wizara kwa kupitia Wataalam wake ilikokotoa gharama na kujiridhisha kwamba kwa bei ya Dola 18.5 kwa ratili mradi hauwezi kuendeshwa kwa faida. 

Hivyo, Wizara iliwasilisha maombi ya Kampuni kwenye Bodi ya Ushauri ya Madini ambayo ilikaa tarehe 19/04/2017 ili kujadili maombi hayo na kisha kumshauri  Waziri mwenye dhamana kwa mujibu kifungu Na. 69 – (3) cha Sheria ya Madini ya mwaka 2010 kwani   Waziri wa Nishati na Madini ndiye mwenye mamlaka ya kutoa ridhaa ya maombi husika.

Tunapenda kuutaarifu Umma kuwa, utekelezaji wa ombi la kampuni ya Mantra la kusitisha uchimbaji wa madini ya urani  kwa muda bado halijakamilika hadi hapo ridhaa itakapotolewa na Waziri mwenye dhamana.

Kuhusu madai ya kuwa Ombi la usitishaji wa uchimbaji limetokana na mabadiliko katika Sheria ya Madini ni upotoshaji kwani sababu za kuomba usitishaji huo ni za kiuchumi zilizotokana na kushuka kwa bei ya Urani kwenye soko la dunia.
Imetolewa na:-
Kitengo cha Mawasiliano Serikalini
Wizara ya Nishati na Madini
Julai 12, 2017

Post a Comment

Find Us On Facebook

TANGAZA NASI LEO