WAZIRI wa Fedha na Mipango, Dk. Phillip Mpango, ameupongeza Mfuko wa Pensheni wa PPF na Jeshi la Magereza kwa kuitikia wito wa Serikali wa kuwekeza kwenye viwanda.

Amesema Mfuko huo kwa kushirikiana na Magereza pamoja na Mifuko mengine ya Hifadhi ya jamii, imeonesha dhamira ya dhati ya kuiunga mkono Serikali ya awamu ya tano, kufanikisha lengo lake la kuwa na uchumi wa viwanda kutokana na uwekezaji mzuri ambao umeanza kutekelezwa na taasisi hizo.

Dkt. Mpango alisema hayo mwishoni mwa wiki, alipokuwa kwenye ziara ya kutembelea kiwanda cha viatu Karanga kilichopo Moshi Mkoani Kilimanjaro pamoja na kujionea maendeleo ya mradi wa kiwanda kipya cha viatu, ambavyo vinatekelezwa kwa ubia baina ya Mfuko wa PPF na Jeshi la Magereza.

Katika ziara hiyo, aliambatana na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Watu Wenye Ulemavu, Jenista Mhagama, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni, Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Profesa Adolf Mkenda na Kamishna Mkuu wa Jeshi la Magereza Nchini, Dk. Juma Malewa.

Waziri Dkt. Mpango alisema kwa niaba ya Serikali anaupongeza Mfuko wa PPF na Jeshi la Magereza pamoja na Mifuko mengine yote ya Hifadhi ya jamii, kwa kuitikia wito wa Serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Magufuli ya kuwekeza kwenye viwanda.

“Uwekezaji ambao unafanywa na PPF kwa kushirikiana na Jeshi la Magereza ndio njia pekee ambao utalikomboa Taifa katika dimbwi la umasikini,” alisema Dkt. Mpango.

Alisema amefurahishwa kuona hatua zimeanza na huku akisisitiza kuwa ratiba iliyopangwa ibakiye kama ilivyo kwamba ukarabati wa kiwanda cha viatu mpaka kufikia mwezi Desemba, mwaka huu, uwe umekamilika.

Dkt. Mpango alisema shauku ya Watanzania ni kuona sasa wanavaa viatu vinavyozalishwa nchini, kwa ngozi na watu wa Tanzania wenyewe.

“Naendelea kuwatia moyo PPF na Magereza pale ambapo wataona pana changamoto yoyote ile, Serikali iko tayari kusaidia hasa kwenye masuala ya kodi ama manunuzi ya umma,” alisema.

Alisema lengo la Serikali ni kuhakikisha adhma yake ya kufikia uchumi  wa kati inafanikiwa kwa haraka iwezekanavyo ili Watanzania waweze kufaidika.

Kwa upande wake, Jenista alisema Serikali imefuraishwa na uwekezaji uliofanywa na Mfuko huo kwa kushirikiana na Jeshi la Magereza katika ukarabati wa kiwanda hicho.

Alisema kiwanda hicho ambacho kinazalisha viatu 150 kwa siku, ukarabati wake utakapokamilika kitazalisha viatu 400 kwa siku.

Jenista alisema wakati umefika sasa wa kuwepo kwa kiwanda cha ngozi kutokana na Tanzania kuwa ni nchi ya pili kwa kuwa na mifugo mingi, na pia itasaidia kuongeza ajira zaidi ya laki mbili.

Naye, Mkurugenzi Mkuu wa PPF, William Erio, alisema ujenzi wa kiwanda kipya ambacho kitakamilika mwaka 2018, utagharimu zaidi ya sh. bilioni 54. 4.

Alisema kiwanda hicho kitachakata ngozi kiasi cha futi za mraba 3,750,000 na kuzalisha viatu milioni 1,200,000 na soli kiasi cha jozi laki tisa, pamoja na bidhaa zingine za ngozi 48,000 kwa mwaka.

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Utafiti wa Maendeleo ya Viwanda Nchini, Profesa Madundo Mtambo, alisema shirika hilo limepewa jukumu la kuusimamia mradi huo na ambao utakapokamilika utakuwa na manufaa makubwa kwa taifa.

mwishoPost a Comment

Find Us On Facebook

TANGAZA NASI LEO