CHAMA cha Mapinduzi katika wilaya ya Bunda mkoani Mara, kimepitisha azimio la kumkataa mkuu wa wilaya hiyo, Lydia Bupilipili, na kumuomba Rais Dk. John Magufuli, kumhamishIa katika wilaya nyingine, kwa madai kuwa hawana imani naye, kwa sababu hatekelezi wajibu wake ipasavyo na atakwamisha shughuli za maendeleo.
Chama hicho kimesema kuwa pia hana mahusiano mazuri na chama, madiwani wa halmashauri zote mbili za wilaya hiyo pamoja na wananchi kwa ujumla.
Pia halmashauri kuu ya CCM imekataa kupokea taarifa ya utekelezaji ya Ilani ya uchaguzi ya kipindi cha miezi sita iliyowasilishwa na mkuu huyo wa wilaya ya Bunda, kwamba inayo mapungufu mengi.
Hayo yamejili juzi kwenye kikao cha halmashauri kuu ya CCM wilayani Bunda kilichofanyika katika ukumbi wa Herieth mjini hapa.
Katika kikao hicho wajumbe kwa asilimia kubwa walisema kuwa hawana imani na mkuu huyo wa wilaya, hivyo ni vyema rais Magufuli akamhamishia katika wilaya nyingine.
Mwenyekiti wa CCM katika wilaya ya Bunda, Justine Rukaka, pamoja na katibu wa siasa na uenezi Bonaventur Jasper, walisema kuwa kikao cha halmashauri kuu ya CCM wilaya hiyo kimefikia hatua hiyo, baada ya kutokuridhika na utendaji kazi wake.
Walisema kuwa wajumbe wote wamekubali mapendekezo yote yaliyotolewa na kamati ya siasa ya wilaya hiyo ya kumkataa mkuu huyo wa wilaya ya Bunda.
“Leo kilikuwa ni kikao cha kuipokea taarifa ya utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi ya chama, lakini taarifa hiyo ilikuwa na mapungufu mengi sana. Taarifa hiyo ilikuwa na vitu ambavyo havikuwa sahihi na siyo vya kweli na vimepotosha serikali.
“Na kwenye kikao cha tarehe 16 mwezi wa kwanza 2018, kamati ya siasa ya chama ambayo mkuu wa wilaya ni mjumbe, ilimtaka ahudhurie kusudi tuweze kuainisha miradi ambayo chama kingependa kuona. Kuna miradi yenye kero, kuna miradi ambayo haitekelezeki, miradi ambayo imechukua muda mrefu bila maelezo, lakini yeye hakutaka kuja.
“Na ametuchagulia miradi ambayo anaitaka yeye, kwa hiyo kamati ya siasa tukaona yeye hataki kuja kwenye kamati ya siasa na ametupuuza na siyo mara moja ni zaidi ya mara mbili. Tunamuita hatoi udhuru yeye anasema mpaka aandikiwe yeye ni rais wa Wilaya, kwa hiyo tukaona hana ushirikiano na chama kwa hiyo tumeona hakuna sababu ya kuendelea kuwa naye.
“Kwa hiyo kamati ya siasa ya Wilaya ilitoa maazimio kwamba itumike busara, mkuu wa Wilaya kwa sababu amekosa mahusiano na chama, amekosa mahusiano na madiwani wa halmashauri zote mbili na hana mahusiano na watumishi wake, basi tunaomba itumike busara ahamishwe aende Wilaya nyingine’ alisema Rukaka.
Katibu wa siasa na uenezi wilayani hapa Bonaventur Jasper, alisema kuwa pia mkuu wa wilaya amekuwa hahudhurii kwenye vikao vya kamati ya siasa bila ya kutoa taarifa.
Aidha, alisema kuwa pia hana ushirikiano na chama na hivyo anaweza kukiweka katika wakati mgumu kwenye chaguzi za serikali za mitaa na uchaguzi mkuu mwaka 2010.
Alisema kuwa wajumbe wa kikao hicho wanamuomba rais ambaye ni mwenyekiti wa chama hicho taifa kufanya busara na kumhamishia sehemu nyingine kwa madai kuwa kwa Bunda ameshindwa kutekeleza wajibu wake ipasavyo, ikiwa ni pamoja na kuwasilisha taarifa ya utekelezaji isiyojitosheleza na yenye mapungufu makubwa.
Baadhi ya wanachama wa CCM wilayani hapa, akiwemo mwenyekiti wa halmashauri ya Mji wa Bunda Abrahamu Mayaya na diwani wa kata ya Manyamanyama Mugendi Makanyanga, walisema kuwa maamuzi hayo yako sahihi, huku wengine wakisema kuwa angepewa nafasi ya kusikilizwa kwanza badala ya kumhukumu, bila ya kupata maelezo yake licha ya kuwepo kwenye kikao hicho.
Hata hivyo katika kikao hicho mkuu huyo wa wilaya ya Bunda hakupatiwa nafasi ya kujitetea ambapo waandishi wa habari walimfuata ofisini kwake na kusema kuwa hakupewa nafasi ya kujitetea, lakini yeye ni mwa CCM mtiifu ingawa hajatendewa haki na kuongeza kuwa hajawahi kuandikiwa barua ya kwenda kwenye kikao cha kamati ya siasa.
“Baadaye zikaibuka hoja dhidi ya DC walisema eti wameshawaandikia barua viongozi mbalimbali wa chama na serikali kunisema mimi…..lakini pamoja na hayo yote mimi ni mwanachama wa chama cha mapinduzi, tena mwanachama mwaminifu, mtiifu na mzalendo kwa hiyo sina la kusema zaidi, viongozi watapima wenyewe” alisema Bupilipili.
Mwisho


Post a Comment

Find Us On Facebook

TANGAZA NASI LEO