Balozi wa China nchini, Mh. Wang Ke (wa tatu kulia) akisalimiana na mwakilishi wa mgeni rasmi Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Uwekezaji  wa Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Aristide Mbwasi (kulia) mara baada ya kuwasili ukumbini wakati wa hafla maalumu ya chakula cha jioni kwa wateja wa benki hiyo wa makampuni ya China nchini Tanzania iliyofanyika katika hoteli ya Serena jijini Dar es Salaam. Wengine katika picha ni Ofisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya Standard Chartered nchini, Sanjay Rughani (wa pili kulia), Mjumbe wa Bodi ya Standard Chartered nchini, Ami Mpungwe (wa pili kushoto) na Mkuu wa Mahusiano na Masoko wa Benki ya Standard Chartered, Juanita Mramba (kushoto).


CHINA katika kipindi cha miaka mitatu ijayo inatarajia kuwekeza katika viwanda 200 nchini Tanzania vitakavyokuwa na uwezo wa kuajiri moja kwa moja Watanzania laki mbili.
Kwa sasa uwekezaji wa China nchini Tanzania umetoa fursa za ajira za moja kwa moja  150,000 na zisizokuwa za moja kwa moja 350,000.
Taarifa hiyo imetolewa na Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Mh. Charles Mwijage katika hafla  ya chakula cha jioni kwa wawekezaji kutoka China iliyoandaliwa na Benki ya Standard Chartered.
Aidha Waziri Mwijage alisema amefurahishwa na kauli iliyotolewa na Benki hiyo kwamba inawekeza dola za marekani bilioni 20 sawa na fedha za kitanzania trilioni 40 katika kampeni ya China ya uwezeshaji mitaji na biashara kutoka Asia kwenda nchi nyingine za dunia.
Kampeni hiyo inayoitwa One Belt One Road inagusa nchi 65, Tanzania ikiwamo.
Aliisifu Benki hiyo kwa kuandaa hafla hiyo kwa wateja wake wa China ikiwa ni sehemu moja ya kutangaza kampeni  hiyo ya China na kuwafanya wananchi wengi kuelewa fursa zinazoambatana nazo.
Alisema kwa sasa Tanzania inapigana kuingia katika uchumi wa kati unaoendeshwa na viwanda na kampeni ya China inakwenda sawa na mpango wa maendeleo wa miaka mitano uliokazania uwekezaji katika viwanda.
Alisema kwa sasa Serikali inaweka vyema mazingira ya uwekezaji na ikiwa na uchumi unaokua kwa kasi wa asilimia  6 hadi 7 juhudi za Benki hiyo za kuonesha fursa za uwekezaji na uendeshaji wa uchumi  zinakaribishwa na serikali ya Tanzania.
Aidha katika hotuba hiyo iliyosomwa na Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Uwekezaji  wa Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Aristide Mbwasi  alisema kwamba mpango huo wa China unaozungumzia uwezeshaji wa mitaji na biashara kutoka Asia kwenda nchi nyingine ni kichocheo cha kukua kwa chumi mbalimbali duniani na kutaka watanzania kushiriki kikamilifu.
Awali Ofisa Mtendaji Mkuu wa Benki hiyo nchini Tanzania, Sanjay Rughani  alisema kwamba Benki ya Standard Chartered duniani inawekeza katika Belt and road Initiative kiasi cha dola bilioni 20 sawa na  shilingi trilioni 44.8 za Kitanzania kuwezesha miradi mbalimbali kwenye kampeni hiyo ya China.
Alisema mwaka jana pekee benki hiyo iliingiliana mikataba katika miradi 40 kwenye nchi mbalimbali za mradi huo.
“Standard Chartered imewekeza katika nchi 45 za kampeni ya belt and Road zenye msukumo mkubwa wa shughuli zikiwemo nchi za Kusini Mashariki mwa Asia, Kusini mwa Asia na Afrika” alisema na kuongeza kuwa kazi yao kubwa ni kutoa mitaji ya kifedha ikiwamo mikopo na kuwezesha miamala mbalimbali.

Aidha alisema asilimia 50 ya mikataba hiyo na shughuli zilizofanywa kwa mwaka 2017 zilikuwa Afrika huku asilimia 25 zikienda Kusini mwa Asia na nyingine ni katika maeneo mbalimbali ya kampeni.
Alisema pamoja na kuishiriki moja kwa moja pia benki ya Standard imekuwa ikishirikiana na taasisi nyingine za fedha kusaidia wateja mbalimbali wa kwenye kampeni hiyo.
Alitaja washirika wao wengine kuwa AIIB, Silk Road Fund, China Development Bank, China Exim Bank na benki nyingine za kibiashara za China.
Alisema ikiwa na historia ya miaka 150 na kuaminika vya kutosha na wateja mbalimbali wamekuwa wakitumia utaalamu na elimu waliyonayo katika kutengeneza mazingira bora ya uwekezaji katika nchi zinazohusika na kampeni ya mitaji kutoka asdia kwenda nchi nyingine.
Rughani alisema  benki  hiyo ina madawati katika nchi mbalimbali yanayoshughulikia wawekezaji kutoka China kwa lengo la kuwawezesha kutambua mazingira ya uwekezaji katika nchi husika na kuwafanya wawe na uhakika na uwekezaji wao.
Katika hafla hiyo ambayo pia ilihudhuriwa na Balozi wa China nchini Tanzania, Wang Ke alisema kwamba taifa lake linaendelea kutoa ushirikiano mkubwa kuwezesha maendeleo kwa nchi washirika katika kampeni iliyoanzishwa takribani mikaa mitatu iliyopita ambayo inakwenda hadi mwaka 2020.
Alisema amefurahishwa sana na juhudi za Benki hiyo katika kutumia fursa iliyonayo kuhamasisha uwekezaji na kuwezesha China na washirika wake wa maendeleo kuwa na uhakika na shughuli na fursa za uwekezaji kwa kuzingatia kampeni ya One Belt One Road.
Biashara ya China na mataifa hayo 65 katika kampeni hiyo, ilizidi dola za Marekani trilioni 3 kati ya mwaka 2014 hadi 2016 na kwamba uwekezaji wa moja kwa moja wa China katika nchi hizo umepita dola za Kimarekani bilioni 129 kufikia mwaka 2016 kutoka dola bilioni 92 mwishoni mwa mwaka 2014.

Post a Comment

Find Us On Facebook

TANGAZA NASI LEO