·
Yawakumbusha
waombaji kuandaa nyaraka muhimu
·
Mwongozo wa
kina kutolewa mwanzoni mwa Mei, 2018
Jumanne, Aprili 17, 2018
Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu
ya Juu (HESLB) inapenda kuwataarifu wananchi kuwa inatarajia kuanza kupokea
maombi ya mikopo ya elimu ya juu kwa mwaka wa masomo 2018/2019 kuanzia wiki ya
kwanza ya mwezi ujao (Mei, 2018) baada ya kukamilishwa kwa maboresho makubwa ya
mfumo wa uombaji kwa njia ya mtandao.
Maboresho ya mfumo
wa maombi
Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB Bw.
Abdul-Razaq Badru (pichani) amesema katika taarifa yake leo (Jumanne, Aprili
17, 2018) kuwa maombi yote yatapokelewa kwa njia ya mtandao (www.olas.heslb.go.tz)
ambao umefanyiwa maboresho na Kituo cha Kompyuta cha Chuo Kikuu cha Dar es
salaam (UCC-UDSM).
Aidha, Bw. Badru amesema dirisha
hilo la litafunguliwa sambamba na kutangazwa kwa mwongozo wa kina utakaotoa
utaratibu wa kuwasilisha maombi, tarehe ya mwisho ya kuwasilisha maombi, sifa
na vigezo vitakavyotumika katika kuchambua na kutoa mikopo kwa mwaka ujao wa
masomo unaotarajiwa kuanza mwezi Oktoba, 2018.
“Tunawasihi wale wote wanaotarajia
kuomba mkopo wa elimu ya juu kusoma kwa makini mwongozo tutakaoutoa kwa vyombo
vya habari na tovuti mwanzoni mwa mwezi Mei, 2018 na kuuzingatia,” amesema Bw.
Badru.
Bw. Badru amefafanua kuwa wito wa
Bodi ya Mikopo umetolewa kutokana na uzoefu wa miaka iliyopita ambapo waombaji
wa mikopo waliwasilisha maombi yao bila kuzingatia mwongozo uliotolewa na
kusababisha baadhi ya wanafunzi kukosa mikopo.
“Mwaka jana, kwa mfano, zaidi ya
waombaji 10,027 kati ya waombaji zaidi ya 61,000 hawakuambatisha nyaraka muhimu
kama vyeti vya kuzaliwa au hata vile vya vifo vilivyothibitishwa na Wakala wa
Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA) kama tulivyoelekeza,” amesema.
Nyaraka muhimu zinazohitajika
Nyaraka nyingine muhimu ambazo
waombaji mikopo wanapaswa kuziandaa ni pamoja na nakala za vyeti vya
kitaaluma za kidato cha nne, sita na stashahada ambazo zimethibitishwa na
Kamishna wa Viapo yaani Wakili au Hakimu.
Aidha, wanafunzi waombaji wenye
ulemavu au wenye wazazi wenye ulemavu wanapaswa kuwa na barua zinazothibitisha
ulemavu huo kutoka kwa Mganga Mkuu wa Mkoa, Wilaya au Kituo cha Afya cha
Serikali;
Bw. Badru ameongeza kuwa wanafunzi
ambao walifadhiliwa katika masomo yao ya Sekondari au Stashahada (Diploma) wawe
na barua za uthibitisho wa udhamini huo kutoka katika taasisi zilizogharamia
masomo yao.
Maafisa wa HESLB
kutoa elimu mikoani
Katika hatua nyingine, Bw. Badru
amesema mwaka huu maafisa wa Bodi ya Mikopo watatembelea mikoa mbalimbali ili
kukutana na waombaji mikopo kwa lengo la kuwaelimisha waombaji mikopo kuhusu
taratibu sahihi za kuwasilisha maombi yao ya mikopo kwa njia ya mtandao. Ratiba
na maeneo itakapofanyia mikutano hiyo itatangazwa mwanzoni mwa mwezi Mei,
2018.
HESLB ilianza kazi rasmi mwaka 2005
ili, pamoja na majukumu mengine, kutoa mikopo ya elimu ya juu kwa watanzania
wahitaji na wenye sifa na kukusanya mikopo iliyoiva ambayo ilitolewa na
Serikali tangu mwaka 1994/1995.
Imetolewa na:
Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu
ya Juu
DAR ES SALAAM
Kwa ufafanuzi: +255 (0) 757 500800
Post a Comment
Post a Comment