KATIKA Kata ya Kipara mtua, Tarafa ya Naipanga , Wilaya ya Nachingwea kiasi cha kilometa 34 kutoka mji wa Nachingwea uliopo mkoani Lindi un...
KATIKA Kata ya Kipara mtua, Tarafa ya Naipanga , Wilaya ya Nachingwea kiasi cha kilometa 34 kutoka mji wa Nachingwea uliopo mkoani Lindi unakutana na eneo maarufu katika ukombozi wa bara la Afrika, Farm 17.
Historia ya Farm 17 inaanzia miaka ya 1947 baada ya Vita Kuu ya Pili ya Dunia, wakati Serikali ya wakoloni wa Uingereza ilipoona inafaa kuwatafutia askari wake eneo la ajira kwa kuwakopesha wapiganaji hao fedha na kuanzisha mashamba ya karanga eneo la Nachingwea kupitia kampuni ya John Molem.
Kupitia mpango huo mashamba 18 yalianzishwa yakipewa majina kuanzia Farm one hadi Farm 18. Hata hivyo kutokana na sababu mbalimbali mashamba hayo hayakuendelea na Waingereza hao kuamua kuondoka na kwenda kuishi Afrika ya Kusini.
Ni katika eneo hili ambalo hivi sasa kuna shule ya Sekondari iliyoazishwa na wananchi yalikuwa ni makazi ya waliokuwa wapigania uhuru kutoka nchi za Kusini mwa Afrika, zikiwamo Msumbiji, Angola na Afrika ya Kusini ambazo kwa miaka kadhaa zilihenyeshwa na wareno na makaburu waliokuwa wakiendesha siasa za ubaguzi wa rangi, pia Zimbabwe ambayo iikuwa chini ya utawala wa Waingereza na baadae muasi Ian Smith hadi 1980 ilipopata uhuru wake.
Hapa ni mahali walipowahi kuishi viongozi wa wapiganaji wa vita vya ukombozi wakiwamo Rais Zimbabwe, Robert Mugabe na viongozi wawili wa Msumbiji ambao wote ni marehemu kwa sasa, Edward Mondlane na mrithi wake, Samora Machel.
Kwa maana hiyo, unapozungumzia harakati za uhuru au ukombozi Kusini mwa Afrika ambazo kwa kiasi kikubwa ziliongozwa na Tanzania chini ya Hayati Mwalimu Nyerere, huwezi kukosa kutaja wilaya ya Nachingwea, hususan eneo la Farm 17.
Katika eneo hili ndipo kulikozaliwa askari jasiri waliofundwa ambao walipelekwa mastari wa mbele nchini msumbiji, Zimbabwe na Angola kufanya vitu vilivyowalazimisha wakoloni kuketi meza moja kuzungumzia uhuru.
Ni rahisi kufika eneo hili ukiwa unatokea Dar es salaam ingawa kutokana na maboresho makubwa katika barabara nyingine zinazokupeleka Nachingwea. Ukitoka dar es salaam unakuwa umekata umbali wa kilometa 614.1 na kwa kutumia basi unaweza kuchukua saa hadi nane.
Umaarufu wa eneo hili la Farm 17 umeanzia mbali, ukianzia na mji wenyewe wa Nachingwea ambapo katika miaka ya 1950 ilipitwa na reli inayokwenda katika mashamba ya karanga mojawapo likiwa ni hilo la Farm 17 ambalo lilibadilishwa kuwa ngome ya wapigania uhuru.
Kiukweli Nachingwea ina mambo mengi ya kujivunia kwa mujibu wa Mkuu wa wilaya, Mohamed Hassan Moyo lakini kubwa ni kuwa mji wa ukombozi katika kusaidia nchi nyingi kujikomboa na kujipatia uhuru.
Akinakiliwa na tovuti ya wilaya hiyo, Mkuu huyo wa wilaya alisema mojawapo ya shughuli ambayo ni nguzo muhimu kwa Wilaya ya Nachingwea hasa katika kuchangia uchumi wa Taifa, wilaya na mtu mmoja mmoja ni utalii na utalii wenye hisia kubwa ni wa shamba hilo ambalo limezalisha wapigania uhuru lakini pia likiwa na historia ya kilimo cha karanga na reli.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Nachingwea, Injinia Chionda Alli Mfaume akizungumza kwa njia ya simu anasema kimsingi Mji wa Nachingwea unasikika kutokana na historia yake ya ukombozi. Mji huu ulihifadhi wapigania uhuru wa nchi za Msumbiji, Angola, Namibia, Afrika kusini na Zimbabwe na uliwatoa salama viongozi wa matraifa ya Msumbiji, Zimbabwe na namibia ambao walikuwa wanatumia makao hayo kama ngome yao.
"Kuna historia nzuri sana ya watanzania na walimwengu wengine kujifunza. Tumefungua eneo hili kwa utalii wa ndani kwa sababu bado tunaendelea kuzungumza na wadau wengine kuimarisha maeneo haya ya zamani hasa mahandaki" anasema Mfaume.
Anasema eneo hilo lenye historia njema ya harakati za kupigania uhuru ni eneo ambalo limejaa historia pevu na linastahili kuhifadhiwa na wilaya ya Nachingwea kwa kutumia vyanzo vyake inafanya kila linalowezekana ili miundombinu yake ikikamilika iwe kivututio si kwa watalii wa ndani pekee bali na jumuiya ya kimataifa inayotaka kujua mahali ambapo wapigania uhuru walisukwa kijeshi na kisiasa kukomboa nchi zao.
"Tulifanya tamasha kubwa katika eneo hili la Farm 17 wakati wa Siku ya utalii duniani, lengo letu lilikuwa kuweka wazi eneo hili na pia kuhimiza utalii wa ndani na kuelezea changamoto tunazokumbana nazo katika kuhifadhi eneo hili ili watu wengi zaidi wajitokeze kuona fahari ya uhifadhi" anasema Mfaume.
Anasema wamefanya mazungumzo na balozi wa Msumbiji nchini waliotembelea eneo hilo pamoja na balozi wa Zimbambwe nchini Tanzania, Balozi Lt. Gen.(Mstaafu) Anselem Nhamo Sanyatwe mwenye sifa ya pekee kabisa kwamba alishawahi kuishi katika shamba hilo hivyo lipo moyoni mwake.
Anasema balozi huyo alitembelea Farm 17 hivi karibuni na kuelezea jinsi anavyolifahamu na kusema Tanzania kupitia rais wa kwanza wa Tanzania Mwalimu Julius Nyerere ilikuwa ni sehemu ya uhuru wao na Tanzania hakika ni nyumbani kwao.
Balozi Anselem anasema alikuwa mmoja ya askari 6,000 wa Zimbambwe waliopata mafunzo eneo la kambi ya Farm 17 baada ya kuondoka kwa wapiganaji wa Msumbiji mwaka 1975 .Anasema makundi ya wapiganaji wa Zimbabwe yaliingia Farm 17 mwaka 1976.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mfaume, balozi alionesha nia ya kushirikiana na halmashauri katika kuhifadhi eneo hilo.
Ingawa Wizara ya Michezo,Utamaduni na Sanaa kupitia programu ya urithi wa ukombozi wa nchi za Afrika @urithiwaukombozi imeanza juhudi zao za kukusanya, kuweka kumbukumbu, kuhifadhi na kuendeleza historia ya ukombozi wa Afrika iliyotokana na harakati za kupigania uhuru, wao Nachingwea kwa nafasi waliyonayo wanataka kulitumia eneo hilo kukuza kipato na pia kuhifadhi historia hiyo adhimu.
Katika eneo hilo la kumbkumbu ya wapigania uhuru kumeanzishwa shule ya sekondari ya Farm 17 ikiwa na lengo la kuendelea kuhifadhi majengo mbalimbali yaliyokuwa yakitumika kama Ofisi za utawala,Maghala ya chakula,Maghala ya silaha, Jiko na kumbi
Nyumba za walinzi na viongozi,Mahandaki na Nyumba ya Samora Machel, rais wa kwanza wa Msumbiji huru aliyekufa katika ajali ya ndege.
"Farm 17 ni eneo jema kwa wale ambao wanapenda kujua hasa msingi wa mapambano kusini mwa Afrika namna watu walivyofunza na kujihami. Hapa pana majengo mbalimbali japo mengine mengine yanatumika kwa shule ya sekondari na shule ya msingi, lipo jengo moja ambalo lilijengwa na Rais Samora kama ngome yake wakati wa vita vya Msumbiji.," anasema Mfaume.
Anasema kinachofurahisha ni namna jengo hilo la chini kwa chini, lilivyoungwa kama barabara ilitumika kuelekea uwanja wa ndege uliokuwa jirani.
"Ukiingia ndani unaona eneo zima,unaona ngome ya kujificha na maadui wakati wa vita na hii ndio ilivyokuwa wakatika wa mapambano kati ya wapigania uhuru na vikosi vya wareno," anasema Mfaume.
Kulikuwa na kila sababu ya eneo hili kujengwa kivita na kingome zaidi kwani kilometa 110 kutoka Nachingwea mjini palikuwa na makambi ya wakimbizi wa Msumbiji eneo la Matekwe na haikujulikana kama wote walioingia hapo ni wale wanaoifagilia Frelimo au kuna maajenti wa wareno.
Ukitafuta historia ya eneo la Matekwe katika mtandao unakutana na simulizi za mzee Salumu Mohamed Migomba akisema kwamba watu walianza kufika eneo hilo kwa kuletwa na serikali mwanzoni mwa miaka ya 1960. Anasema watu walianza kujenga mji hadi pale miaka ya 1967 alipofika waziri mkuu wa Tanzania wakati huo Mzee Rashid Mfaume Kawawa kuwaomba wananchi kuwapokea wageni kutoka Msumbiji wasiopungua 15,000.
Ukifika eneo la Matekwe utakayakuta majengo tofauti ambayo yalitumiwa na wakimbizi, viongozi na majengo ya shughuli za jamii wakati huo ambayo hadi sasa yanaendelea kutumiwa kama ofisi za kijiji, zahanati, kanisa, shule. Baada ya Msumbiji kupata uhuru Juni 25, 1975 mambo mengi ya hapa yalibadilika katika maeneo hayo mawili.
Ikumbukwe kwamba Samora alichaguliwa kuwa kiongozi baada ya kuuawa kwa Mondlane kiongozi wa kwanza wa Frelimo kwa bomu lilikuwa katika barua.
Mwalimu Longnus Nambole , Mkuu wa kwanza wa sekondari ya Farm 17 anasema kwamba kuna kila sababu ya serikali na wadau wengine kushirikiana kutunza eneo hilo kwani.
Pamoja na kuwa na majengo ya kambi za wapigania uhuru, kazi hiyo ilipomalizika awali yaligeuzwa kuwa chuo cha kufundishia wanajeshi. Chuo hiki kilikuwa kinatoa mafunzo kwa maafisa kwa jeshi kutoka nje ya nchi pamoja na mafunzo ya awali kwa askari wanaoanza. Desemba 1992 chuo hicho kilivunjwa na kuhamishiwa Mgulani Dar es salaam.
Farm 17 hakika ni kumbukumbu njema na kama eneo hilo litaboreshwa, litazalisha ajira kwa wananchi lingevuta watalii kutoka maeneo mbalimbali Duniani na pia kuchangia pato la taifa.
Imeandikwa na: Rahel Pallangyo
COMMENTS