.Bandari yavuka lengo upokeaji shehena .Meli zaingia kwa kasi kutokana na ufanisi . Meli kubwa ya watalii kubwa kuja kesho Na Beda Msimbe ...
.Bandari yavuka lengo upokeaji shehena
.Meli zaingia kwa kasi kutokana na ufanisi
. Meli kubwa ya watalii kubwa kuja kesho
Na Beda Msimbe
MABADILIKO katika miundombinu, teknolojia ya kupakua na kupakia shehena na kasi ya kuhudumia meli katika Bandari ya Dar es Salaam kumeifanya bandari hiyo kuendelea kuaminika na hivyo kupokea meli nyingi zenye ukubwa stahiki katika biashara ya bandari .
Aidha katika mwaka huu wa fedha 2023/2024 bandari hiyo imevuka lengo la nusu ya kwanza kwa kushughulikia shehena ya tani milioni 12 kati ya lengo walilopangiwa la tani milioni 22.
Kauli hiyo imetolewa na Mkurugenzi wa Bandari ya Dar es Salaam, Mrisho Mrisho wakati wa kufanya majumuisho na kundi la waandishi wa habari ambao walitumia zaidi ya saa mbili kutembelea bandari hiyo yenye gati 12.
Alisema pamoja na kwamba walipangiwa lengo la serikali la tani milioni 22 wao kama Bandari wamepanga lengo la kuhudumia shehena ya tani milioni 24 na wanahakika watalivuka lengo hilo kutokana na mipango yao na pia kuwapo kwa ufanisi katika uhudmiaji wa meli.
Alisema mwaka wa fedha wa 2022/2023 walipangiwa lengo la kuhudumia tani milioni 19.6 za shehena lakini wao kutokana na mipangilio mizuri ya kazi walifanikiwa kuhudumia tani milioni 21.46, wakivuka lengo walilopewa kwa tani milioni 2. Pia alisema kwa mwaka 2021 walihudumia tani milioni 18 za shehena.
“Tunajua tunaweza kuvuka lengo kutokana na mazingira ambayo tunayo sasa ikiwamo ya kuwepo na uwezo wa kuingiza katika bandari meli kubwa zaidi na kuwa na vifaa vya kisasa vya kuhudumia shehena hasa makasha” alisema Mrisho.
Alisema wao kama Bandari wanafurahi sana kuwa na meli za kuhudumia wakati wote kwani inawasaidia kutekeleza majukumu yao kwa taifa na majirani wanaotumia bandari hiyo.
“Mizigo kwenda nje ni asilimia 60 na imekuwa ikiongezeka kwa asilimia 20 kila mwaka hivyo uwapo wa meli ukisubiri unatupa changamoto ya kuongeza kasi na ufanisi” alisema Mrisho ambaye alijinasibu kuwa kazi iliyofanywa na bandareo zote za TPA kwa mwaka wa fedha 2022/2023 wa kukusanya tani milioni 24 za shehena, utafanywa na Bandari ya Dar es Salaam pekee mwaka huu.
Alisema kutokana na kukamilika kwa miundombinu muhimu kama upanuaji wa mlango Bahari sasa wanauwezo wa kupokea meli za mita zaidi ya 300.
“Bandari yetu ilizoea kupokea meli zenye urefu wa mita 263 baada ya maboresho lakini sasa uwezo umeongezeka zaidi baada ya kukamilika kwa kazi ya upanuzi wa mlango bahari. Na Jumanne (kesho) tutapokea meli ya watalii yenye urefu wa mita 294 na itafungwa katika gati namba moja hadi tatu” alisema Mrisho.
Mrisho alisema kuwa uwapo wa ufanisi ndio unafanya meli ziongezeke katika bandari hiyo, akitolea mfano wa asubuhi ya jana kwamba hadi kufikia mchana walikuwa wamezihudumia meli tano na kuziondoa bandarini ikiwamo iliyobeba magari yapatayo 2,500 na kupisha meli nyingine iliyoleta magari 1,500.
Bandari ya Dar es Salaam ina uwezo wa kupokea na kuhifadhi magari 6,000 kwa wakati mmoja.
Ukitaka kujua tunafanya vizuri katika uhudumiaji meli kuanzia tarehje 12 hadi 15 tutapokea zaidi ya meli 16 na ukija kesho naweza kukuambia kwamba idadi ya meli zinazosubiri zinafikia 40, alisema Mrisho na kuongeza kuwa kinachojalishwa sio tu ongezeko la meli bali na kasi ya kuzihudumia.
“Sisi ndio lango la biashara hivyo tuna mipango ya haraka ya muda mfupi na ya muda mrefu kuhusu ufanisi wa bandari ikiwamo ya ujenzi wa gati nyingine tano kwa upande huu ambao sisi tunaita terminal, lakini pia mazungumzo ya kiserikali yanaendelea kwa bandari kutwaa eneo la Kamandi ya Maji ili kutengeneza gati zingine” alisema Mrisho wakati akitembeza waandishi wa habari kuwaonesha shughuli zinazofanyika katika gati mbalimbali na kuzitolea maelezo.
Kwa mwaka wa fedha 2022/23 bandari hiyo ilipokea magari 300,000.
Alisema kuna mitambo mipya ya upakuaji na upakiaji makasha ambayo inahitaji umeme wa kipekee wa Kv33 ambayo ipo tayari bandarini (imesimikwa) inasubiri umeme huo ili kuongeza kasi ya upakuaji na upakiaji wa makasha.
“Tumepangiwa kuhudumiwa makasha milioni 1.2 tumejizatiti kwa hilo kwa kuwa na mitambo hii” alisema wakati waandishi walipofika katika gati 5-8 ambazo zilikuwa zinaendeshwa na TICS” alisema Mrisho.
Akizungumzia upakuaji wa mafuta alisema kwa sasa wana vituo vitatu vya kupokea mafuta na kimoaj kikitumika kupakia mafuta na kwamba wa sasa Bandari inafikiria kujenga gati litakalotumika kupakua mafuta na kupunguza muda zaidi wa ungojeaji unaotokana na changamoto nyingi za kiforodha.
“Tukimaliza gati hili na matangi yetu meli itapakua mafuta na kuingiza katika matangi hayo na habari za kiforodha na matakwa mengine ya kisheria yatakuja baadae” alisema.
Akizungumzia mikakati ya kuendelea kuboresha ufanisi wa bandari hiyo na kupunguz Amuda wa meli kukaa maji makuu amesema bandari imepanga kujenga magati namba 12 hadi 15 yenye urefu wa mita 300 kila moja, Kujenga kituo cha lojistiki Kurasini ambao shughuli zinazohusu upakuaji na upakiaji zitafanyika, kuongeza matumizi ya bandari kavu ikiwamo ya Kwala.
Alisema mradi uliobadili kabisa Bandari hiyo ni wa DMPD ambayo iliwezesha kuongeza gati na kina cha maji kuanzia mita saba hadi mita 14.5 na hivyo kuwezesha meli kubwa kupiga gati moja kwa moja.
mwisho
COMMENTS