Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete ametumia siku nzima Ijumaa, Mei 9, 2014, kutembelea kiwanda k...
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya
Mrisho Kikwete ametumia siku nzima Ijumaa, Mei 9, 2014, kutembelea kiwanda
kikubwa zaidi cha saruji kuliko kingine chochote duniani cha Dangote Cement
Obajana Plant na kinachomilikiwa na tajiri mkubwa zaidi wa Afrika, Bwana Aliko
Dangote, ambaye pia anajenga kiwanda kikubwa cha saruji mjini Mtwara.
Akiandamana na Waziri wa Viwanda na Biashara, Mheshimiwa
Abdallah Kigoda, kwa siku nzima, Rais Kikwete ametembelea kiwanda hicho cha
Saruji cha Dangote kilichoko katika eneo la Obajana, Jimbo la Kogi,
kilomita 400 kaskazini mashariki mwa mji maarufu wa kibiashara wa Nigeria,
Lagos.
Rais Kikwete ambaye alikuwa nchini Nigeria kuhudhuria
Kongamano ya Uchumi Duniani-Afrika (WEFA) mwaka huu aliamua kutumia siku yake
ya mwisho ya ziara yake ya siku tatu nchini humo, kwa kutembelea uwekezaji
mkubwa wa mwekezaji ambaye ameanza ujenzi wa kiwanda cha saruji cha Mtwara
ambacho kitakuwa kiwanda kikubwa zaidi cha saruji kuliko kingine chochote
katika Tanzania, kikiwa na uwezo wa kuzalisha tani za kimetriki milioni tatu
kwa mwaka.
Rais Kikwete ambaye amepokelewa kwenye Uwanja wa Ndege wa
Kiwanda hicho na Bwana Dangote mwenyewe, ameanza ziara yake kwa kutembelea
machimbo ya kiwanda hicho ambayo yako kilomita tisa kutoka kiwandani ambako
malighafi ya kiwanda hicho husafirishwa kwa madaraja na mikada maalum hadi
kiwandani.
Bwana Dangote amemwambia Rais Kikwete kuwa kwa sasa Kiwanda
cha Obajana kinazalisha tani za kimetriki milioni 10.25 kwa sasa kwa mwaka na
hivyo kukifanya kiwanda hicho kuwa kiwanda kikubwa zaidi cha saruji duniani
kilichoko katika eneo moja na kuwa baada ya upanuzi unaoendelea kufanywa kwenye
kiwanda hicho, uwezo wake wa uzalishaji utaongezeka na kufikia tani za
kimetriki 13.0 kwa mwaka ifikapo mwakani 2015.
Bwana Dangote amemwambia Rais Kikwete kuwa kiwanda hicho
kilicho kwenye eneo la kilomita za mraba saba kitakuwa kimegharimu kiasi cha
dola za Marekani bilioni 2.5 wakati upanuzi wake utakapokamilika. Kwa sasa
kiwanda hicho kina biashara ya dola za Marekani bilioni mbili kwa mwaka.
Bwana Dangote amemwambia Rais Kikwete kuwa kiwanda hicho
kilichoanza kujengwa mwaka 2003 na kukamilishwa mwaka 2006 na hatimaye
kuzinduliwa na Rais Olusegun Obasanjo Mei 12, mwaka 2007, wiki mbili kabla ya
kustaafu Urais wa Nigeria, kinaajiri watu 800 kwa wakati mmoja na hivyo kuwa
miongoni mwa waajiri wakubwa zaidi katika Nigeria.
“Mheshimiwa Rais, ili kuelewa vizuri mchango wa kiuchumi na
kijamii za kiwanda hiki na viwanda vyetu vingine katika maeneo mengine ya
Nigeria, unahitaji kukumbuka kuwa kabla ya kuanza kujenga kiwanda hiki, Nigeria
nzima ilikuwa na uwezo za kuwazalisha tani za kimetriki za saruji milioni1.5
tu, wakati huo chini ya miaka 10 iliyopita. Tunataka kufikia hatua ya
kuhakikisha kuwa eneo la Afrika Magharibi na hata Bara letu la Afrika linaacha
kabisa kuagiza saruji nje ya Bara letu. Na tutafikia huko.”
Mbali na Kiwanda cha Obajana, Kampuni ya Saruji ya Dangote
inazalisha saruji katika maeneo mengine mawili ya Nigeria ambalo uzalishaji wa
jumla wa maeneo hayo matatu ni tani za metriki 20.25 kwa mwaka.
Amesema Bwana Dangote kuwa ili kuweza kuwa na uhakika wa
umeme, uongozi wa kiwanda hicho uliamua kuzalisha umeme wake kwa ajili ya
kiwanda hicho kwa kujenga, miongoni mwa hatua nyingine, bomba ya kilomita 92 la
kusafirisha gesi kutoka Ajaokuta hadi kwenye kiwanda hicho.
Alipoulizwa na Rais Kikwete kama wanategemea kwa namna
yoyote umeme wa taifa, Bwana Dangote alijibu kwa furaha, “hatujaunganishwa kwenye
gridi ya taifa na tunadhani hili ni jambo zuri kwa sababu hatua tulizochukua
zinatuhakikishia umeme wakati wote na kwa kiwango ambacho tunakihitaji.
Tunatumia gesi ama diseli yetu wenyewe. Na wala siyo umeme tu, hata miundombinu
ya eneo hilo kiliwemo daraja hili kubwa linalonganisha eneo la machimbi na
kiwanda, tumejenga sisi Mheshimiwa Rais.”
Bwana Dangote amesema kuwa mbali na kujenga miundombinu ya
umeme wake, kiwanda hicho pia kimejenga bwawa lake lenyewe kwa ajili ya huduma
ya maji kusaidia uzalishaji wa saruji bila kutegemea huduma ya maji ya
Serikali. Aidha, bwawa hilo linatoa huduma ya maji kwa jamii inayozunguka
kiwanda hicho.
Mbali na shughuli za kiwanda, Kampuni ya Bwana Dangote
inashiriki kwa karibu sana shughuli za jamii inayozunguka kiwanda ambacho kwa
sasa imeanzishwa miji midogo saba katika eneo lililokuwa pori lenye nyumba 50
za wenyeji tu kabla ya shughuli za kiwanda hicho kuanzishwa.
Bwana Dangote amemwambia Rais Kikwete kuwa kampuni yake
inatoa shughuli za elimu, maji na umeme kwa wananchi ambao wanazunguka kiwanda
ambacho tokea kuanzishwa kwake limevutia mabenki 13 ambayo yameanzishwa matawi
yake katika eneo la kiwanda. “Mheshimiwa Rais, mbali na nyumba za wafanyakazi,
tunawajengea hata nyumba za kuishi wananchi wanaozunguka eneo hili ambao
wanatuunga mkono sana.”
Mbali na kutoa huduma nyingine za kijamii, Kampuni ya Saruji
ya Dangote inajenga taasisi kubwa ya elimu ya Dangote Academy ambayo itatoa
elimu na mafunzo ya kiufundi kwa ajili ya kuandaa wafanyakazi wa kiwanda hicho
na watoto wa jamii inayozunguka kiwanda hicho.
Ili kuhakikisha kuwa upanuzi wa kiwanda hicho unakwenda kwa
kasi kubwa zaidi, Bwana Dangote ameagiza kiasi cha malori 6,000 kutoka China
kusaidia ujenzi na pia amechukua uamuzi usiokuwa wa kawaida wa kuagiza maelfu
ya vibarua kutoka nchi hiyo hiyo ya China kushiriki katika ujenzi huo na
kuumaliza kwa haraka.
Bwana Dangote amemwambia Rais Kikwete kuwa kampuni yake
inafanya jitihada kubwa kuhakikisha kuwa Rais Kikwete anakifungua kiwanda
cha saruji cha Mtwara kabla ya kustaafu mwishoni mwa mwaka ujao.
Mbali na Nigeria na Tanzania, Bwana Dangote ana viwanda ama
anajenga viwanda vya saruji ama na shughuli za saruji katika nchi 14 za Afrika
ikiwamo Ethiopia, Zambia, Mozambique, Kenya, Senegal na Sierra Leone, Afrika Kusini,
Congo (Brazzaville), Cameroun, Ghana, Liberia na Ivory Coast.
Rais Dkt Jakaya
Mrisho Kikwete akitembezwa kwenye machimbo ya kiwanda cha saruji cha Dangote
Cement Obajan Plant kilichoko kilomita 400 Kaskazini Mashariki mwa Lagos
alipotembela May 9, 2014
|
Mbali na shughuli za uzalishaji wa saruji, Bwana Dangote
ambaye anakubaliwa kuwa tajiri mkubwa zaidi katika Afrika kwa thamani ya dola
za Marekani bilioni 25 yeye na kampuni yake ya Dangote Group pia ina shughuli
za uzalishaji wa sukari, uzalishaji wa chumvi, utengenezaji wa magunia,
uzalishaji maji, uzalishaji wa vyakula vya aina mbali mbali, uzalishaji wa
mafuta ya kupikia, utengenezaji wa nyanya. Kwa sasa anaendelea na ujenzi wa
kiwanda cha mbolea na kile cha kuzalisha bidhaa za petrol na kemikali.
Kampuni ya Saruji ya Dangote – Dangote Cement- ndiyo kampuni
kubwa kuliko zote katika Afrika Magharibi kwa sasa ikiwa na thamani ya dola za
Marekani bilioni 22.7 kwa tathmini ya mwaka huu baada ya kuongeza thamani yake
kutoka dola za Matrekani bilioni14.5 za mwaka jana.
Mwishoni
mwa ziara hiyo yenye mafanikio makubwa, Rais Kikwete ameondoka Obajana kurejea
nyumbani kupitia Kinshasa, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na Luanda, Angola
ambako kesho (jumamosi) anatarajia kukutana na marais wa nchi hiyo kabla ya
kurejea nyumbani
COMMENTS