*Achukua fomu CCM na kusema; “Chema chajiuza *Atamba ana uwezo wa kutosha kuiongoza nchi *Ni nguli wa sheria, mwanajeshi na ki...
*Achukua fomu CCM na kusema; “Chema chajiuza
*Atamba ana uwezo wa kutosha kuiongoza nchi
*Ni nguli wa sheria, mwanajeshi na kiongozi wa dini
*Atamba ana uwezo wa kutosha kuiongoza nchi
*Ni nguli wa sheria, mwanajeshi na kiongozi wa dini
JAJI Mkuu Mstaafu wa
Tanzania, Augustino Ramadhani (70) ambaye kwa sasa ni Rais wa Mahakama ya
Afrika, amepandisha joto la urais ndani ya CCM, baada ya jana kuchukua fomu ya
kuomba kuteuliwa na chama hicho kupeperusha bendera ya CCM katika uchaguzi mkuu
wa Oktoba mwaka huu.
Mara baada ya kuchukua
fomu, Jaji Ramadhani ambaye pia ni mwanajeshi aliyestaafu akiwa na cheo cha
Brigedia Jenerali, kiongozi wa dini akiwa Mchungaji wa Kanisa Anglikana na
mwanamichezo mahiri, alisema amejitokeza kwa kuwa ana uwezo wa kutosha katika kuongoza
nchi.
Pia ameahidi kuyaangalia
mapendekezo ya wananchi yaliyoachwa kwenye Katiba inayopendekezwa iwapo atapata
ridhaa ya kuongoza nchi kwani katiba ni ya wananchi.
"Sina makeke ndiyo
maana nimeongozana na watu wachache kuja kuchukua fomu, siku zote chema
chajiuza," alisema.
Alisema yeye ni mtu safi
na hajawahi kutajwa mahali popote kuhusika na ufisadi kutokana na kuwa na
mapenzi wa kuitumikia nchi yake na atahakikisha anashughulika na tatizo la
rushwa na ufisadi katika nchi.
Akiwa ameongozana na mkewe,
Saada Mbarouk Ramadhani ambaye ni mwanajeshi wa ngazi ya juu mwenye cheo cha Luteni Kanali, alisema ana uzoefu wa kutosha
ndio maana anaomba dhamana ya chama na wananchi ili aweze kuwa kiongozi mkuu wa
nchi.
"Nina vigezo vya
kutosha na nia uwezo najiamini, nataka nipate nafasi ya kuteuliwa na chama na
baadaye niwe kiongozi mkuu wa Nchi ili
kwa pamoja tuijenge nchi yetu," alisema
Jaji Mstaafu Ramadhani,
tofauti na wagombea wengine zaidi ya 35 waliomtangulia kuchukua fomu CCM,
hakujieleza, bali alitaka kuulizwa tu maswali na waandishi wa habari.
"Mimi sikuitisha
kikao cha kutangaza nia ninataka waandishi waniulize maswali tu," alisema.
Alipoulizwa kama anaona
kuna mgombea yeyote ambaye ni tishio kwake alisema, yeye ni Brigedia Jenerali
hawezi kuogopa chochote.
Pia alipohojiwa akiwa
rais atawezaje kuondoa tatizo la rushwa na ufisadi na hata tatizo la mauji ya watu wenye ulemavu
wa ngozi, alisema matatizo hayo yote yatatafutiwa dawa mapema kwani hata alipokuwa
Jaji Mkuu alizunguka mikoa 15 ambapo alikutana na wakuu wa mikoa na wilaya na
walizungumzia suala hilo.
"Suala la rushwa na
ufisadi ni mtoto pacha sheria zipo ni utekelezaji tu unaotakiwa," alisema.
Alisema tatizo la mauaji
ya walemavu wa ngozi serikali inajitahidi na wale waliohusika wamefikishwa
mahakamani wengine wamehukumiwa adhabu ya kifo na kinachosubiriwa ni
utekelezaji wa adhabu hizo.
Alisema elimu zaidi
inatakiwa kutolewa ili wananchi wafahamu viungo vya albino havileti utajiri.
Pia alipohojiwa kwamba, wakati
akiwa kama Makamu Mwenyekiti wa Tume ya Marekebisho ya Katiba kuna mapendekezo
ya wananchi yaliachwa, atafanyaje akipata nafasi ya kuongoza nchi?
Alijibu kwa kusema Katiba
ni ya wananchi si ya kwake, na atasikiliza matakwa ya wananchi kama wakihitaji
yarudishwe basi yatarudishwa.
Alipohojiwa amekuwa
mwanachama wa CCM tangu lini alisema ameingia kwenye siasa mwaka 1969. Alisema
alikuwa mwanachama wa Umoja wa Vijana wa TANU tangu Agosti, mwaka 1969 wakati
huo akiwa mwanafunzi wa Sheria katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Akiwa chuoni wakati
akikaribia kumaliza shahada yake akatuma maombi ya kujiunga na jeshi na na
akaulizwa kama ni mwanachama wa TANU akasema ni mwanachama wa Vijana wa TANU
akaambiwa lazima awe mwanachama wa Tanu ndipo ajiunge na Jeshi.
Alisema alikwenda
kufuatilia kadi ya TANU na alifanikiwa kuipata na aliendelea kuwa na mwanachama
wa CCM hadi mwaka 1992 wakati mfumo wa vyama vingi vya siasa ulipoanza na Katiba
kukataza Majaji kuwa wanachama wa vyama vya siasa.
Jaji Mstaafu Ramadhani
alisema alipostaafu Ujaji mwaka 2011 alirudi tena na kuwa mwanachama wa CCM. Pia alipopata tu shahada ya chuo kikuu alijiunga
na jeshi moja kwa moja na mwaka 1971 aliteuliwa kuwa Luteni Usu kwa alikaa
makao makuu ya Jeshi na ilipoanzishwa Brigedi ya Faru mkoani Tabora.
Alisema Rais wa Zanzibar wakati huo, Mzee Aboud Jumbe
alimuita arudi Zanzibar ili awe mwanasheria mkuu lakini alitaka kujifunza kwanza kabla ya
kushika nafasi hiyo.
Mwaka 1978 akawa Naibu
Jaji Mkuu wa Zanzibar na wakati wa Vita baina ya Tanzania na Uganda alikwenda vitani
na alirejea Zanzibar mwishoni mwa mwaka 1979 na ndipo akateuliwa kuwa Jaji Mkuu
wa Zanzibar.
Alipotoka Zanzibar
aliteuliwa kuwa Jaji wa Mahakama ya Rufaa Nchini kwa miaka 20, baadaye Jaji Mkuu
miaka mitatu na nusu akastaafu na sasa ni Rais wa wa Mahakama ya Haki za
Binadamu Afrika.
Historia yake
Jaji
Augustino Ramadhani alizaliwa Desemba 28, 1945 mjini Unguja, Zanzibar akiwa
mtoto wa pili kati ya wanane waliozaliwa kwa wazazi wake. Baba yake ni Mathew
Douglas Ramadhani, raia wa Zanzibar aliyefariki dunia mwaka 1962 na mama yake, Bridget Ramadhani
alifariki dunia mapema mwaka huu.
Watu
wengi hushangaa kuona au kusikia ana majina mawili ya dini tofauti. Augustino
(jina la Kikristo) na Ramadhani (jina la Kiislamu). Lakini ukweli wa mambo ni
kuwa yeye ni Mkristo wa dhehebu la Anglikana na ni mchungaji wa kanisa hilo.
Elimu
ya msingi aliianzia wilayani Mpwapwa Mkoa wa Dodoma katika Shule ya Msingi
Mpwapwa mwaka 1952 -1953 darasa la kwanza na la pili. Baadaye alihamia mkoani
Tabora na kusoma darasa la tatu na la nne katika Shule ya Mingi “Town School”
mwaka 1954 – 1956. Mwaka 1957 – 1958 alisoma darasa la la sita na la saba
katika Shule ya Msingi Kazel Hill (sasa inaitwa Shule ya Msingi Itetemia), kabla
ya kurudi Mpwapwa ambako alikamilisha darasa la nane mwaka 1959.
Aijiunga
na Shule ya Sekondari ya Wavulana Tabora mwaka 1960-1965 kwa ajili ya elimu ya
kidato cha kwanza na nne pamoja na elimu ya kidato cha tano na sita. Baada ya
kumaliza elimu ya sekondari alipata fursa ya kujiunga katika Chuo Kikuu cha Dar
es Salaam akianza kusomea Sheria. Shahada hii nyeti aliisoma kuanzia mwaka 1966
hadi alipohitimu Machi 1970 na baada ya kuhitimu alijiunga na Jeshi la Kujenga
Taifa kwa mujibu wa sheria na aliajiriwa katika Jeshi la Wananchi Tanzania
(JWTZ), kufanya kazi za uanasheria.
Kwa
mtu mwenye shahada ya chuo kikuu enzi za miaka ya 1970, kupanda vyeo kilikuwa
kitu cha lazima. Jeshi halikuwa na wasomi wengi kama ilivyokuwa katika sekta
nyingine na kila aliyekuwa na elimu kubwa alikuwa mtu muhimu.
Ndiyo
maana haikushangaza kwamba mwaka 1971 tayari alikuwa Luteni (nyota mbili) akiwa
kambi ya Mgulani na miaka sita baadaye akahamishiwa Brigedi ya Faru mkoani
Tabora wakati huo akiwa tayari ni Meja.
Kutoka
hapo, alifanya kazi jeshi na uraiani kwa vipindi tofauti hadi alipostaafu na
sasa kujiona ameshakomaa katika nyanja nyingi, hivyo yuko tayari kuvaa viatu
vya Rais wa Awamu ya Nne anayemaliza muda wake, Rais Jakaya Kikwete.
Anakuwa Mzanzibari wa
tatu kujitosa Urais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania mwaka huu, wengine
wakiwa Mtoto wa Mwasisi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Balozi Ali Karume na
mwanadiplomasia aliyewahi kuwa Waziri wa Fedha wa Zanzibar na Waziri wa Mambo
ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Tanzania, Amina Salum Ali ambaye kwa sasa
ni Balozi wa Umoja wa Afrika (AU) huko Marekani.
SOURCE: Sifa Lubasi, HabariLEO Dodoma
COMMENTS