Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dkt Medard Kalemani amezindua Kituo cha kudhibiti mfumo wa umeme wilayani Chato mkoani Geita na kuwaeleza wananchi kuwa matatizo ya umeme wilayani humo yamefikia tamati.

Akizungumza mjini humo mara baada ya kuzindua Kituo husika Julai 5 mwaka huu, Dkt Kalemani ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Chato alisema kuwa, matatizo kwenye laini ya Biharamulo hayataiathiri tena Chato kama ilivyokuwa ikitokea awali na vivyo hivyo matatizo kwenye laini ya Chato hayataiathiri Biharamulo..

“Kabla ya ujenzi wa Kituo hiki, tatizo lolote kwenye sehemu yoyote ya laini, ingefanya wateja wote wakose umeme hivyo kukamilika na kufunguliwa kwa Kituo hiki, kutafungua neema mpya katika Wilaya na Mkoa wetu,” alisema Dkt Kalemani.

Naibu Waziri Kalemani alisema kuwa, lengo la Serikali ni kuhakikisha kunakuwa na umeme wa kutosha unaosafirishwa ili kuwafikia wananchi wengi zaidi kwenye maeneo yao ili waweze kutumia nishati hiyo kuboresha maisha yao.

“Hii itasaidia kuongezeka kwa kipato cha mtu mmoja mmoja, pia kuwepo kwa huduma bora za kijamii kama vile kwenye vituo vya afya na Zahanati, Maabara, Shuleni pamoja na uanzishwaji wa Viwanda vidogovidogo.”

Aidha, Naibu Waziri alifafanua kuwa, kwa kuwa azma ya Serikali ya awamu ya Tano ni uendelezaji na uanzishwaji wa Viwanda vipya, Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa maendeleo, imewekeza kwenye miradi mikubwa ya uzalishaji na
usafirishaji umeme.

Aliitaja baadhi ya miradi iliyokamilika hivi karibuni kuwa ni pamoja na Mradi wa Kinyerezi – 1 wenye uwezo wa kuzalisha megawati 150 kwa kutumia gesi asilia.
Vilevile, alisema kuna miradi mikubwa ya ujenzi wa njia za kusafirishia
umeme ukiwemo unaojengwa kuanzia Iringa hadi Shinyanga, maarufu kwa
jina la ‘Backbone’ ambao unasafirisha umeme kwa msongo wa kilovolti 400
na kwamba unatarajiwa kukamilika hivi karibuni pamoja na vituo vikubwa vya
kupozea umeme.

Akizungumzia utekelezaji wa Mradi wa REA (Umeme Vijijini) Awamu ya Pili, Dkt Kalemani alisema kuwa Mradi ulianza mwezi Februari mwaka 2014 na kwamba unahusisha ujenzi wa kilomita 266.5 za njia ya msongo wa kilovolti 33 na kilomita 216 za msongo wa njia ndogo ya kilovolti 0.4 kwa gharama ya Dola za Marekani 8,205,368.81 pamoja na fedha za Kitanzania shilingi 3,023,317,202.

Alieleza kuwa, Mradi huo utanufaisha Wilaya za Chato, Geita na Mbogwe ambapo jumla ya vijiji 59 vitanufaika na jumla ya wateja 7272 walitarajiwa. “Mpaka kufikia Juni 30 mwaka huu, jumla ya wateja 2509 walikuwa wameunganishwa.”

Dkt Kalemani alifafanua kuwa, Mkandarasi amekamilisha ujenzi wa njia
ya msongo wa kilovolti 33 kwa asilimia 98 na anaendelea na ujenzi kwenye wigo
ulioongezwa ambazo ni kilomita 73.5 za msongo wa kilovolti 33. Mpaka sasa
amejenga kilomita 39 ambapo kwa njia ya msongo wa kilovolti 0.4 amejenga
kwa asilimia 92.

Naibu Waziri alilipongeza Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) kwa juhudi
zake za kuimarisha miundombinu ya umeme nchini na kuhakikisha wananchi
wanapata umeme bora na wa uhakika.

Akitoa wito kwa Shirika hilo,aliwaagiza watendaji wote wa Tanesco kubadili utendaji wao kwa kuhakikishawao ndiyo wanawafuata wateja mahali walipo badala ya kusubiri wateja wawafuate ofisini.

“Mkiwafuata wateja itasaidia kupunguza kero mbalimbali na pia kuwarahisishia ninyi kufahamu sehemu mbalimbali zenye matatizo na kuyashughulikia mara moja,” alisisitiza.

Awali, akimkaribisha Naibu Waziri kuzindua Kituo hicho cha kudhibiti
mfumo wa umeme, Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco, Mhandisi Felchesmi Mramba alisema kuwa, Mradi huo umesanifiwa na kujengwa na Wahandisi wa ndani wa Tanesco kwa gharama ya shilingi 758,544,046 ambazo ni fedha za ndani za Shirika hilo.

Mhandisi Mramba alisema kuwa, Mradi umegawanyika sehemu kuu mbili ambazo ni ujenzi wa njia ya usambazaji umeme yenye urefu wa kilomita 3.5 ya msongo wa kilovolti 33, ufungaji wa mashine poozeo (Transfoma) mbili zenye ukubwa wa kilovoti 200 na kilovolti 50 pamoja na ujenzi wa njia ndogo ya msongo wa kilovolti 0.4 yenye
urefu wa kilomita 0.5 katika eneo la Makao Makuu ya Wilaya.

Alisema, sehemu nyingine ni ujenzi wa nyumba ya kuongezea mitambo (control room) pamoja na ufungaji wa mitambo ya kukata umeme (circuit breakers) za msongo wa kilovolti 33.
SOURCE;mem weekly news

Post a Comment

Find Us On Facebook

TANGAZA NASI LEO